Casemiro apigwa chini Brazil

Muktasari:

  • Staa huyo wa Manchester United amewekwa pembeni Brazil itakayocheza michuano ya Copa America katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi.

MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO Casemiro amepigwa chini kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Brazil siku chache tangu alipocheza kwa kiwango cha hovyo katika kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Crystal Palace.

Staa huyo wa Manchester United amewekwa pembeni Brazil itakayocheza michuano ya Copa America katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi.

Casemiro, aliyekuwa nahodha wa Brazil mwaka jana, si pekee kwenye orodha ya mastaa waliokosekana kwenye kikosi cha wachezaji 23 wa kocha Dorival Junior. Mchezaji mwenzake kwenye kikosi cha Man United, Antony naye hayumo sambamba na straika wa Tottenham Hotspur, Richarlison na fowadi wa Arsenal, Gabriel Jesus wote wamepigwa chini.

Casemiro ndiye mchezaji aliyeshtua kwa kuwekwa kando katika kikosi hicho kutokana na kiungo huyo mwenye umri wa miaka 32, kuwa kwenye kikosi cha Brazil karibu kwa kipindi chote cha soka lake.

Kiungo huyo mkabaji amecheza mechi 75 kwenye kikosi cha Selecao na alikuwa mtu muhimu kwenye kikosi hicho wakati wa fainali mbili za Kombe la Dunia na tatu za Copa America. Lakini, staa huyo wa zamani wa Real Madrid amekuwa kwenye kiwango kibovu siku za karibuni huko Man United, ikiwamo mechi ya wiki iliyopita, ambapo timu yake ilikumbana na kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Palace huko Selhurst Park.

Kutokana na Man United kuwa na majeruhi wengi sehemu ya ulinzi kocha Erik ten Hag alimrudisha Casemiro kwenye nafasi ya beki wa kati, eneo ambalo ameshindwa kabisa kulitendea haki.