CAF yatangaza ratiba fainali za Afcon

Muktasari:
- Morocco na Comoros watafungua michuano hiyo Desemba 21, 2025 kwa mchezo wa Kundi A kwenye uwanja mpya wa Complexe Sportif Prince Moulay Abdellah huko Rabat, wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 69,500.
Shirikisho la Soka la Barani Afrika (CAF) limetangaza ratiba ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika nchini Morocco 2025, ambazo zitachezwa kwenye viwanja tisa katika miji sita tofauti.
Morocco na Comoros watafungua michuano hiyo Desemba 21, 2025 kwa mchezo wa Kundi A kwenye uwanja mpya wa Complexe Sportif Prince Moulay Abdellah huko Rabat, wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 69,500.
Rabat itakuwa na viwanja vinne vya mechi, huku miji mingine ya wenyeji ikiwa ni Casablanca, Agadir, Marrakech, Fes na Tangier, ambapko kila mji utakuwa na uwanja wake mmoja.
Mechi nne za robo fainali zitachezwa kwenye Uwanja wa Complexe Sportif Prince Moulay Abdellah huko Rabat, pamoja na viwanja vya Tangier, Marrakech na Agadir.

Nusu fainali zitachezwa Rabat na Tangier, huku mechi ya kumaliza nafasi ya tatu itafanyika kwenye Uwanja wa Stade Mohammed V huko Casablanca.
Kutakuwa na mechi 52 kwa kipindi cha siku 29, zikiwa ni sikukuu ya soka kwa mashabiki zinazoonyesha ustadi na shauku ya soka la Afrika.
Morocco, inayosherehekea kuwa mwenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika la TotalEnergies kwa mara ya kwanza tangu 1988, pia inajiandaa kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la FIFA 2030, ambako itakuwa mwenyeji mwenza pamoja na Ureno na Hispania, huku pia Argentina, Paraguay, na Uruguay zikiandaa mechi pia katika kusherehekea miaka 100 ya michuano ya Kombe la Dunia la FIFA, ambayo ilifanyika kwa mara ya kwanza huko Uruguay mwaka 1930.