Bruno: Hakuna namna lazima tubadilike
Muktasari:
- Man United inapitia upepo mbaya na Bruno anawakumbusha nyota hao, wako kwenye timu kubwa na presha ni lazima na iuli waweze kubadili mambo ni lazima wabadilike na wawe majasiri.
MANCHESTER, ENGLAND: HAKUNA namna, lazima tubadilike. Ndivyo anavyosema Nahodha wa Manchester United, Bruno Fernandes, huku akiwataka nyota wenzake kuonyesha kweli wana ujasiri wa ‘kuchezea timu hiyo’, hasa kipindi hiki cha msoto wanaopitia kwenye Ligi Kuu England.
Man United inapitia upepo mbaya na Bruno anawakumbusha nyota hao, wako kwenye timu kubwa na presha ni lazima na iuli waweze kubadili mambo ni lazima wabadilike na wawe majasiri.
Bruno ambaye aliisaidia Man United kushinda mchezo wa Europa League dhidi ya Rangers wiki iliyopita na kuendeleza rekodi yao ya kutopoteza mechi kwenye mashindano hayo, alisema kwa sasa timu haipo katika nafasi inayotakiwa iwe.
Pia alizungumzia kauli ya kocha wake, Ruben Amorim ambaye hivi karibuni alisema huenda hii ndio timu mbovu kuwahi kutokea katika historia ya Man United.
“Hali halisi ni ukiwa unacheza timu hii lazima ukubali kukabiliana na presha, lazima uwe na ujasiri ili ucheze timu hii, ndivyo ilivyo,” alisema Bruno.
“Lazima uhisi kila wakati, kila mchezo ni nafasi mpya ya kuturudisha kwenye nafasi tunayostahili. Kwa bahati mbaya kwetu msimu huu, tumekuwa na mabadiliko mengi, kupanda na kushuka na kila mara tunapoonekana kufika katika nafasi nzuri, tunapigwa tena na kushuka.”
“Tunachopaswa kufanya ni kila tunapopigwa na kuanguka, lazima tuinuke na kujaribu kupigana tena.”
Man United imekuwa katika hali mbaya msimu huu na mchezo wao dhidi ya Brighton uliwafanya kuweka rekodi mbaya zaidi kwa kupoteza mechi nyingi katika uwanja wao wa nyumbani baada ya miaka 131.
“Sitaki kumsikia kocha wangu akisema mambo fulani kuhusu timu kwa sababu najua haamini hivyo, lakini alitafuta namna ya yeye pia kujihusisha na hilo jambo linalowafanya watu wasiwe na hasira au kuvunjika moyo.”
“Anaposema ‘timu mbaya zaidi kuwahi kutoka Manchester,’ anazungumza kuhusu nafasi tuliyopo na ukiangalia tulipo kwenye ligi, tuko kwenye nafasi mbaya zaidi kuwahi kutokea.
“Lazima tukubali hilo, hiyo ndiyo hali halisi, kwa bahati mbaya tumekuwa katika hali hii kwa muda mrefu, na klabu haistahili kuwa hapo. Lakini tunapaswa kukubali hilo na kuelewa tunahitaji kujisukuma kufikia hatua kubwa zaidi na nafasi za juu zaidi.”
Kabla ya mchezo wao wa jana dhidi ya Fulham, Man United ilikuwa ikishika nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu England kwa pointi 26, ilizokusanya baada ya kushinda mechi saba, sare tano na kufungwa 10.