Brazil yamtimua kocha baada ya kichapo, Ancelotti atajwa

Muktasari:
- Brazil inashika nafasi ya nne katika Kundi la Amerika Kusini, baada ya kupoteza michezo mitano kati ya 14, ingawa bado iko katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2026.
Brazil imemtimua kocha Dorival Junior, baada ya kupokea kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa mahasimu wao Argentina katika michuano ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia.
Brazil inashika nafasi ya nne katika Kundi la Amerika Kusini, baada ya kupoteza michezo mitano kati ya 14, ingawa bado iko katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2026.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 62, ambaye amezinoa timu kadhaa za soka za Brazil, alitangazwa rasmi Januari 2024.

Mchezo wake wa kwanza ulikuwa ni ushindi wa 1-0 dhidi ya England katika mechi ya kirafiki iliyochezwa Uwanja wa Wembley, amefanikiwa kushinda michezo saba, sare sita na kupoteza tatu katika michezo 16 aliyoifundisha timu hiyo.
Hata hivyo, Shirikisho la Soka la Brazil (CBF) lilitangaza kumuondoa kocha huyo baada ya kupata kipigo hicho dhidi ya Argentina ambayo imeshafuzu Kombe la Dunia 2026.
"Uongozi unamtakia mafanikio katika safari yake ya baadaye. Kuanzia sasa, CBF inafanya kazi ya kumtafuta mrithi wake," ilisema taarifa fupi ya Brazil.
Dorival, ambaye hakuwahi kuichezea timu ya taifa ya Brazil, umaarufu wake mkubwa ni kuiwezesha Flamengo kushinda Copa Libertadores ya 2022.

Vyombo vya habari vya Brazil vinaripoti kuwa kocha wa Al-Hilal, Jorge Jesus, ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kuwa kocha mpya wa Brazil.
Lakini pia ikiwania kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti ambayo ilimtaka kabla ya kumchagua Dorival.