Bila Shin Guard haya yangewapata wanasoka!

Muktasari:
UGOKO ni moja ya eneo la mwili wa mwanasoka linalokumbana na majanga ya kujeruhiwa kutokana na sehemu hiyo ya mbele chini ya goti kuwa katika hatari ya kugongwa kirahsi wakati wa mchezo.
UGOKO ni moja ya eneo la mwili wa mwanasoka linalokumbana na majanga ya kujeruhiwa kutokana na sehemu hiyo ya mbele chini ya goti kuwa katika hatari ya kugongwa kirahsi wakati wa mchezo.
Eneo hilo linapogongwa huwa na maumivu makali na hii ni kutokana na sababu ya kimaumbile ambayo ni kutokuwa na misuli wala mrundikano wa mafuta na tishu zingine kama ilivyo kigimbi au paja.
Mwanasoka wanapogongwa eneo hilo hugaragara kwa maumivu makali.
Ni vigumu kwa mwanasoka yeyote katika maisha ya uchezaji kutowahi kukumbana na kadhia ya majeraha ya ugoko kutokana na eneo hilo kuhusika na kukurukakara nyingi wakati wa mchezo.
Ili kukabiliana na hatari ya kupata majeraha ya ugoko Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) liliweka mwongozo maalumu kwa wanasoka wote kutakiwa kuvaa kifaa tiba kijulikanacho kama ‘shin guard’.
Hii ilikuwa ni moja ya hatua mathubuti ya kusaidia kupunguza majeraha ambayo huambatana na maumivu makali pale eneo hili linapojeruhiwa.
Bila shin guard wanasoka wangekuwa kila mara wanapata majeraha mbalimbali ikiwamo kujeruhiwa kwa mfupa wa ugoko kwa kuvunjika au kupata nyufa na majeraha ya tishu laini zilizojitandika katika mfupa wa ugoko ikiwamo tendoni na ligamenti.
Kifaa tiba hicho kimekuwa maarufu katika soka kiasi cha wanasayansi kadhaa kuwahi kukifanyia utafiti mara kwa kwa mara ili kubaini kama kweli kina umuhimu kwa wanasoka.
Matokeo mengi ya kisayansi yalikuja na majibu chanya, hivyo kuendelea kuakisi umuhimu wa matumizi kwa wanasoka.
Zipo shin guard za aina tofauti zinazoshindana kwa ubora ikiwamo aina ya Polypropylene inayotengenezwa na Adidas, Mercurial inayotengenezwa na Nike na Carbon fiber inayotengezwa na kampuni zingine.
Kila mtengenezaji amekifanya katika ubora wa hali ya juu ili kuhakikisha kinakidhi matakwa ya mtumiaji na kumsaidia mchezaji kuepukana na mejaraha ya ugoko.
Leo nitawapa ufahamu zaidi wa kifaa tiba hiki na majeraha ya ugoko ambacho kinasaidia kupunguza majeraha ya ugoko.
MAJERAHA YALIVYO
Ni kawaida wanasoka washambuliaji kupenda kukimbia na mpira kwa kasi, huku wakipiga chenga na kuwatoka mabeki wa timu pinzani.
Wanasoka hao hukutana na mabeki ambao hawakubali kushindwa na ambao mara nyingi huwakwatua kwa mtindo wa kuteleza na kupiga kwanja.
Makwanja hayo ya mabeki mara kwa mara hugonga eneo hilo ambalo lipo chini ya mguu - chini ya goti.
Eneo hilo unapolishika kwa mbele unahisi kabisa kushika mfupa uliofunikwa na ngozi na tando zingine za tishu laini. Swali la kujiuliza kwa namna wanavyopigwa makwanja mengi lakini bado wanacheza.
Siri kubwa ya kurudi na kucheza hata baada ya kukwatuliwa au kugongwa eneo la ugoko ni kutokana na uwepo wa shin guard au kwa jina lingine hujulikana kama shin pad.
Kwa Kiswahili kifaa hicho huitwa ‘Kikinga Ugoko’ huwasaidia sana wanasoka kuepukana na majeraha ya ugoko na ndiyo sababu mamilioni ya wanasoka hukivaa ili kuepukana na ajali za ugoko.
Kifaa hicho kinapovaliwa eneo la ugoko hupunguza kuwa katika hatari ya kupata majeraha hayo ya mara kwa mara.
Uzuri wa kifaa hicho kinapatikana kwa urahisi na bei zake kwa sasa ni rahisi, huanzia Sh5,000 kwa bei ya chini. Na huwa katika urefu na ukubwa tofauti.
Wanasoka ndio wahanga wa majeraha ya mara kwa mara katika eneo la chini ya ugoko - sehemu ya mbele hii ni kwa sababu mpira wa miguu unahusisha zaidi miguu.
Ugoko ni mfupa mkubwa wa mguu ambao umeunganika na mfupa mwingine mdogo ambao umejishikiza kwa sehemu ya pembeni, ukiunda eneo la mguu chini ya goti. Sehemu ya mbele ya mfupa huu umefunikwa na ngozi laini, utando wa mafuta machache pamoja na mishikio ya tishu laini ya misuli iliyo kama kitambaa.
Maumbile haya katika eneo la mbele linachangia kuwa katika hatari ya kupata majeraha kirahisi, hii ni kwa sababu ya uchache wa misuli na mrundikano wa mafuta.
Uwepo wa misuli na mafuta pamoja na tishu laini kwa wingi eneo lolote la mwili hutoa ulinzi na kukinga mfupa usifikiwe endapo kitu kitagonga eneo hilo.
Ukilanganisha na sehemu ya mfupa wa ugoko kwa upande wa nyuma ambayo imefunikwa na msuli uliojaa ambayo ndio huitwa kigimbi kutokana na kujaa vizuri, hivyo kuifanya kutopata majeraha kirahisi.
Mfupa huu mkubwa huunganika na mfupa mkubwa wa juu pamoja na tishu laini kuunda ungio la goti. Ungio la goti ndilo ambalo linabeba uzito mkubwa wa mwili.
Ukiacha majeraha ya tishu laini, zipo aina tatu za kuvunjika kwa mfupa wa ugoko ambayo huwa ni sehemu ya juu ambayo mfupa huweza kutoka ufa au kuvunjika vipande viwili na pia unaweza kuvunjika vipande zaidi ya viwili. Sehemu hii pia hukumbana sana na majeraha ya kuvunjika mfupa eneo la katikati. Mara nyingi kuvunjika kwa mfupa wa ugoko huweza kujeruhiwa pamoja na misuli, mishipa ya fahamu na nyama zingine laini.
DALILI NA TIBA
Dalili za majeraha haya huwa ni maumivu makali baada ya kukwatuliwa au kujigonga ama kupigwa, michubuko, kuvimba, kuuma baada ya kutomaswa, kuchechemea, kutohimili mwendo na kupungua ufanisi na kubadilika rangi eneo la jeraha.
Uchunguzi huanzia uwanjani mchezaji alipoumia, baadaye picha za xray na ct scan/MRI hutumika kujua kama mfupa umevunjika au majeraha ya tishu laini.
Matibabu ya huanzia uwanjani kwa kupewa huduma ya kwanza ili kuondoa maumivu na uvimbe.
Kanuni ya kupumzisha, kutumia barafu, kukandamiza na clip bandegi na kunyanyua mguu ndio hutolewa muda mfupi baada ya majeraha haya. Matibabu yatategemea na ukubwa wajeraha na aina yake, mara chache sana upasuaji unaweza kuhitajika. Ni muhimu sana kwa wachezaji wa soka kuvaa vikinga ugoko ili kuepukana majeraha ya mbalimbali ya ugoko yanayoweza kuwaweka nje ya soka kwa muda mrefu.
NA DK SHITA SAMWEL