Benfica yathibitisha ofa ya Neves

Muktasari:
Neves, 19, ni mmoja wachezaji wanagombewa na timu vigogo nyingi Ulaya na huenda akatimka Benfica katika dirisha hili la usajili la majira ya kiangazi.
LISBON, URENO: RAIS wa Benfica, Rui Costa amethibitisha kwamba wamepokea ofa mezani kwa ajili ya Joao Neves, ambaye amekuwa akihusishwa na klabu za Manchester United, Arsenal na PSG.
Neves, 19, ni mmoja wachezaji wanagombewa na timu vigogo nyingi Ulaya na huenda akatimka Benfica katika dirisha hili la usajili la majira ya kiangazi.
Rais wa klabu hiyo, Costa, amethibitisha kwamba klabu hiyo ya Ureno iko katika mazungumzo kuhusu ofa hiyo iliyowasilishwa siku chache zilizopita, na kwamba wanaweza hata kupokea dau chini ya Euro 120 milioni ambayo ndio bei ya kuvunjia mkataba wake iliyopo katika mkataba wake.
Hata hivyo, rais huyo haikuitaja klabu iliyowasilisha ofa hiyo wala kiwango cha pesa kilichowekwa mezani katika ofa hiyo, lakini unaweza kuotea.
Costa alionekana kuizungumzia ofa ya PSG iliyoripotiwa mapema ya Pauni 59 milioni, huku pia ikidaiwa mwezi uliopita kwamba United na Arsenal zilikuwa tayari kuwasilisha ofa.
"Sijawahi kusema kwamba ili Joao Neves aondoke ni lazima iletwe pesa ya kuvunjia mkataba wake tu, madai hayo si ya kweli," Costa alisema kuiambia A Bola.
"Ninachoweza kusema kuhusu Joao Neves ni kwamba kuna ofa mezani ambayo inajadiliwa. Lakini kwa sasa Joao Neves bado ni mchezaji wa Benfica. Hili si jambo ninalotaka kulificha kwa sababu najua mashabiki wa Benfica wanataka kujua kama Joao ataondoka ama atabaki.”