Osimhen akataa pesa za Waarabu

Muktasari:
- Kwa mujibu wa Sky Sport, Napoli wamekataa ofa ya awali kutoka Al-Hilal kwa ajili ya Osimhen ambayo inafikia Euro 70 milioni, kiasi ambacho ni pungufu ya thamani ya mchezaji huyo ambayo inakadiriwa kuwa ni Euro 75 milioni.
NAPLES, ITALIA: LICHA ya mshahara mkubwa uliowekwa mezani kutoka kwa miamba ya Ligi Kuu ya Saudi Arabia, Al-Hilal, Victor Osimhen bado hajashawishika kujiunga nao na ripoti zinaeleza Napoli wamekataa pia ofa hiyo.
Kwa mujibu wa Sky Sport, Napoli wamekataa ofa ya awali kutoka Al-Hilal kwa ajili ya Osimhen ambayo inafikia Euro 70 milioni, kiasi ambacho ni pungufu ya thamani ya mchezaji huyo ambayo inakadiriwa kuwa ni Euro 75 milioni.
Mbali ya Napoli kukataa ofa hiyo, Osimhen naye amekataa ofa ya Al-Hilal ambayo inadaiwa kuwa ni Euro 26 milioni ikiwa pamoja na bonasi.
Mustakabali wa mshambuliaji huyo raia wa Nigeri hadi sasa bado haujajulikana licha ya utitiri wa timu nyingi zinazomhitaji baada ya kuonyesha kiwango bora akiwa na Galatasaray kwa mkopo msimu uliopita akitokea Napoli.
Licha ya kiwango chake, Osimhen na timu zote zinazomhitaji hazijafanya makubaliano yoyote na Napoli au yeye mwenyewe.
Hata Galatasaray pia inataka kumbakisha mshambuliaji huyo kwa kumsainisha mkataba wa kudumu baada ya kuvutiwa na kiwango chake alichoonyesha msimu uliopita ambapo alifunga mabao 37 na kutoa asisti nane katika mechi 41 za michuano yote.
Kutokana na kiwango chake msimu uliopita, aliisaidia timu hiyo kushinda ubingwa wa Super Lig na Kombe la Uturuki, na pia alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Msimu wa Uturuki.
Kwa sasa Osimhen anatarajiwa kurejea Napoli kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya kabla ya kujiunga na timu itakayofikia makubaliano ya kumnunua.