Bayern Munich kuibania Arsenal kwa Sesko

Muktasari:
- Mabingwa hao wa Bundesliga walikuwa wakimnyatia Sesko tangu msimu uliopita na sasa wameanza mazungumzo tena na wakala wake licha ya kufahamu Arsenal pia inamhitaji.
MUNICH, UJERUMANI: BAYERN Munich inaripotiwa kuwa na nia ya kumsajili Benjamin Sesko kama mrithi wa muda mrefu wa Harry Kane.
Mabingwa hao wa Bundesliga walikuwa wakimnyatia Sesko tangu msimu uliopita na sasa wameanza mazungumzo tena na wakala wake licha ya kufahamu Arsenal pia inamhitaji.
Leipzig imeweka wazi wanahitaji kiasi kisichopungua Pauni 75 milioni ili kumuuza Sesko ambaye amefunga mabao 21 msimu uliopita.
Arsenal tayari imefanya mazungumzo ya awali kuhusu uhamisho huo, huku mshambuliaji akiwa kipaumbele kikuu kwenye orodha ya Mkurugenzi wa Michezo Andrea Berta dirisha lijalo.
Tovuti ya Bild inaeleza Bayern imepanga kufanya kila linalowezekana ili kumpata staa huyu licha ya kufahamu Arsenal ndiyo ina nafasi kubwa kwa sasa.
Ikiwa itafanikiwa kumpata Sesko, mpango wao ni kumsogeza Kane nyuma kucheza kama namba 10, nafasi ambayo si ya asili kwake lakini huenda ikamfaa kutokana na tabia yake ya kushuka chini kuchukua mpira.
Mbali ya vigogo hawa wa Ulaya, Al-Hilal kutoka Saudi Arabia pia ilimfuata mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Slovenia lakini kipaumbele chake ni kubaki barani Ulaya.
Sesko amefunga mabao 39 katika mechi 87 tangu ajiunge na Leipzig miaka miwili iliyopita.
Kabla ya kutua Leipzig, Sesko alikuwa akiichezea Red Bull Salzburg ya Austria, timu ambayo aliwahi kupita Erling Haaland kabla ya kuhamia Borussia Dortmund na kisha Manchester City.
Salzburg waliwahi kufanya mzaha mitandaoni dhidi ya Manchester United mwaka 2022 ilipojua kuhusu nia yao kwa Sesko, ambaye wakati huo alikuwa na miaka 19.
“Sasa tunataka Euro 1 bilioni, Bruno Fernandes na Fred kwa ajili ya Sesko,” waliandika Julai 2022.