Bayern inazama, Tuchel kitanzini

MUNICH, UJERUMANI. AJIRA ya kocha Thomas Tuchel imezidi kuingia shakani baada ya mabingwa watetezi wa Bundesliga, Bayern Munich kukumbana na kipigo cha tatu mfululizo katika michuano yote.

Bayern juzi ililala 3-2 ugenini dhidi ya VfL Bochum na licha ya straika wao kinara Harry Kane kufunga bao lake la 29 katika mechi 30 za michuano yote tangu atue Ujerumani, miamba hiyo haikunusurika kichapo.

Kipigo hicho kimeifanya Bayern kuzidiwa pointi nane na vinara Leverkusen ya kocha Xabi Alonso na kutia doa mbio zao za kutetea taji hilo ambalo wamelibeba kwa misimu 11 mfululizo.


NGOMA NGUMU
Kinachoonekana Tuchel anaweza kutimuliwa wakati wowote. Wachezaji wanaonekana kupoteza mwelekeo chini yake, hakuna kinachoenda, na ushindi umekuwa mgumu kupatikana.
Kadi nyekundu ya pili kwa Dayot Upamecano katika mechi mbili, lazima atakuwa yuko ovyo kabisa sasa.
Wachambuzi wanaona hakuna sababu ya kumuanzisha Choupo-Moting badala ya Mathys Tel. Baada ya kuifundisha Bayern Munich kwa mwaka mzima, Tuchel anaonekana bado hajajua namna ya kuvitumia vipaji vilivyojaa katika timu yake.

Harry Kane alifunga juzi, lakini alikuwa na mechi mbaya ajabu. Alikosa mabao ya wazi mno, akapoteza pasi, na hakuonekana kujumuika mchezoni. Alionekana kama kivuli cha mchezaji yule tishio aliyeanza kwa mbembwe nusu ya kwanza ya msimu.

Kama Tuchel ataendelea kubaki madarakani, Bayern Munich inaweza kuchukua muda kurejea makali yake.

Bayern ilianza kupigwa na Leverkusen 3-0 katika Bundesliga, kasha ikalala 1-0 ugenini dhidi ya Lazio katika mechi ya awali ya hatua ya 16-Bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, kabla ya kuchapika tena 3-2 mikononi mwa Bochum wikiendi.


VITA YA TOP 4
Mbali na Leverkusen yenye pointi 58 na Bayern (pointi 50), vita ya Top 4 ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao inazihusisha pia VfB Stuttgart yenye pointi 46 na Borussia Dortmund yenye pointi 41, huku RB Leipzig ikiwanyemelea katika nafasi ya tano ikiwa na pointi 40. Zote zimecheza mechi 22.

FC Koln (pointi 16), Mainz (pointi 15) na SV Darmstadt (pointi 12), ndio zinashika nafasi 3 za mkiani kwenye mstari wa hatari ya kushuka daraja, wakati juu yao nafasi ya 15 yupo Borussia Monchengladbach pointi 22.