Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ripoti yamng’oa beki Yanga

YAO Pict

Muktasari:

  • Lakini, katikati ya hilo huenda kukawa na sapraizi kibao mara tu dirisha la usajili wa wachezaji katika ligi hiyo litakapofunguliwa, kwani majina makubwa yatajikuta yakiachwa na mengine mapya kuingia kutoka ndani na nje ya nchi.

ZILE nyakati za kufanya mambo zimeshafika katika Ligi Kuu Bara, kwani licha ya kwamba msimu bado haujamalizika, lakini timu zimeanza kujiandaa kwa ajili ya msimu ujao zikifanya usajili kimyakimya kusikilizia tu umalizike ili zianze kutangaza majina ya mastaa zinaowasajili.


Lakini, katikati ya hilo huenda kukawa na sapraizi kibao mara tu dirisha la usajili wa wachezaji katika ligi hiyo litakapofunguliwa, kwani majina makubwa yatajikuta yakiachwa na mengine mapya kuingia kutoka ndani na nje ya nchi.


Na wakati ukisoma hayo, siku za beki Yao Kouassi Attouhola ndani ya Yanga ni kama zinahesabika kwa sasa kutokana na ripoti juu ya afya yake akiendelea kujiuguza kutokana na kufanyiwa upasuaji hivi karibuni, kumfungulia njia beki mpya kutoka TP Mazembe, Ibrahima Keita kuja kumalizana na mabosi wa klabu hiyo ya Jangwani.


Ripoti ya kitabibu ya beki huyo wa kulia raia wa Ivory Coast aliyerejea nchini akitokea Tunisia alikoenda kufanyiwa upasuaji wa goti, imemchomoa kikosini, ikielezwa atalazimika kujiuguza kati ya miezi 7-8, kitu ambacho Yanga inaona itapoteza, hivyo kumleta beki mpya wa kuziba pengo.


Kwa hesabu hizo za Yao kukaa nje kwa muda mrefu, zimeifanya Yanga kujua itakosa huduma ya beki huyo kwa zaidi ya nusu msimu na hivyo kujiongeza mapema kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi na mashindano mengine ikiwamo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


Hata hivyo, inaelezwa mabosi wa Yanga bado wana imani na beki huyo endapo atakuwa sawa, lakini ripoti hiyo imewasha taa ya kijani kwamba klabu hiyo iendelee na hesabu za kumalizana na beki wanayempigia hesabu ambaye ni Ibrahima Keita kutoka TP Mazembe anayewindwa pia na Zamalek.


Yanga ilikuwa imebakiza kutuma tiketi tu ili Keita aje nchini haraka kusaini mkataba wa miaka miwili.

Keita anamalizia mkataba alionao Mazembe msimu huu na Mwanaspoti linafahamu kuwa beki huyo amewakimbia mabosi wake kimtindo akidai anarudi nyumbani kutatua matatizo ya kifamilia.


Keita hakuwapo kwenye mchezo wa juzi wa Mazembe dhidi ya Sanga Balende iliposhinda kwa mabao 3-0 kwa ruhusa hiyo, lakini atatua nchini wiki hii kumalizana na Yanga.


“Tumeumizwa sana na ripoti hii ya Yao, kukosekana kwa muda huo ni pigo na ukitazama malengo yetu kwa msimu ujao hatutaki kufanya makosa tena,” alisema bosi mmoja wa juu Yanga aliyeongeza:


“Yao akiwa sawa shughuli yake sote tunaijua, lakini kwa sasa tunataka apone sawasawa, pia malengo yetu yasitetereke tutasajili beki mpya wakati Yao anapona.”


Jeraha ambalo Yao analiuguza liliwahi kumpata pia kipa wa timu hiyo Aboutwalib Mshery, lakini katika hali iliyoshtua madaktari wa timu hiyo alitumia miezi mitatu na nusu kupona sawasawa tofauti na inavyoelezwa kwa Yao ambaye awali alikuwa akisumbuliwa na majeraha ya kifundo cha mguu (ankle).