Bao bora la Messi hili hapa

MIAMI, MAREKANI. SUPASTAA, Lionel Messi amelitaja bao lake analolipenda kati ya mabao yanayokaribia 850 aliyofunga kwenye maisha yake ya soka.
Gwiji huyo wa Argentina, Messi, anatajwa kama mmoja kati ya wanasoka bora wa muda wote. Na rekodi yake ya kufunga imekuwa haina mjadala tangu alipoanza kukipiga akiwa mdogo kwenye kikosi cha Barcelona.
Alifunga mabao 672 alipokuwa na kikosi cha Barcelona, kisha akaongeza 32 akiwa Paris Saint-Germain na mabao 11 katika mechi 14 akiwa Inter Miami.
Ukiweka kando mabao hayo 726 aliyofunga kwenye klabu, Messi amefunga pia mabao 106 kwenye kikosi cha wakubwa cha Argentina na mabao 16 alipokuwa na timu za vijana za taifa chini ya miaka 20 na 23.
Mabao hayo yanahusisha pia aliyofunga kwenye mechi kubwa kama za Ligi ya Mabingwa Ulaya na fainali za Kombe la Dunia. Na amekuwa na mabao ya juhudi binafsi zaidi ya saba ambayo yaliingia kwenye mchakato wa kuwania tuzo ya mabao bora, Puskas Award. Lakini, Messi ametaja bao lake alilopenda zaidi kati ya mabao 848 aliyofunga kwenye maisha yake ya soka.
Na bao hilo ni lile juhudi binafsi aliloifunga Real Madrid katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2011.
“Bao ambalo siku zote nitalikumbuka, ni lile nililofunga dhidi Madrid, tuliipiga 2-0 kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya uwanjani Bernabeu,” alisema Messi.
BAO LENYEWE
Messi alichukua mpira katikati, akagongeana pasi na Sergio Busquets akawazunguka viungo Xabi Alonso na Lassana Diara. Akawalamba chenga Raul Albiol, Sergio Ramos na Marcelo kabla ya kufunga kwa mguu wa kushoto akimtesa, Iker Casillas.