Arsenal yarudisha makali, yaichapa Leeds kwao
Muktasari:
- Wakati ilipoonekana kuwa matatizo ya majeraha kwa Gunners yalikuwa yamepungua, Mikel Arteta alipata wasiwasi mpya baada ya Mikel Merino kuondolewa kutokana na tatizo la mguu na Bukayo Saka kuumia wakati wa mazoezi ya kabla ya mechi.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imekomesha mfululizo wa mechi tatu bila ushindi kwenye Ligi Kuu England baada ya kuibabua Leeds United mabao 4-0 katika Uwanja wa Elland Road, Jumamosi.
Wakati ilipoonekana kuwa matatizo ya majeraha kwa Gunners yalikuwa yamepungua, Mikel Arteta alipata wasiwasi mpya baada ya Mikel Merino kuondolewa kutokana na tatizo la mguu na Bukayo Saka kuumia wakati wa mazoezi ya kabla ya mechi.
Hata hivyo, baada ya kuhimili presha ya awali kutoka kwa wenyeji, Arsenal ilipata mdundo wao na kwenda mapumzikoni ikiwa mbele kwa mabao 2-0, yaliyofungwa na Martin Zubimendi kwa kichwa na bao la kujifunga la Karl Darlow.
Leeds ilionyesha dalili za kurudi kipindi cha pili kilipoanza, lakini matumaini yao yalizimwa na Viktor Gyokeres, aliyefunga katika mechi mbili mfululizo za Arsenal kwa mara ya kwanza pamoja na mshambuliaji mwenzake Gabriel Jesus.
Kikosi cha Arteta sasa kimeongeza tena uongozi wa pointi saba juu ya Manchester City na Aston Villa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England, huku Leeds ikibaki nafasi ya 16, ikiwa pointi sita juu ya timu tatu za mkiani.
Maandalizi ya Arsenal kabla ya mechi hayakuwa mazuri hata kidogo ilikuwa haijashinda katika mechi tatu za ligi. Walikabiliana na Leeds ambao walikuwa hawajapoteza mechi tano mfululizo nyumbani Elland Road, pambano la Jumamosi lilionekana kuwa hatari kwa vinara wa ligi, lakini kikosi cha Arteta kilipuuza changamoto zote na kuimarisha tena matumaini yao ya ubingwa.
Iwe ni kupitia mipira ya adhabu au mchezo wa wazi, mipira ya Arsenal ilikuwa tishio kubwa muda wote wa mechi, na pongezi maalum zinafaa kwenda kwa Madueke, ambaye alijua kuwa anaanza dakika 10 tu kabla ya mechi kuanza, lakini alihusika moja kwa moja katika mabao yote mawili ya kipindi cha kwanza.
Bao jingine la Gyokeres lilikuwa la kukaribishwa, na baada ya Arsenal kushindwa kujibu ushindi wa Manchester City na Aston Villa wiki iliyopita, sasa presha ipo kwa wapinzani wao Man City na Aston Villa katika kupunguza tofauti ya pointi.
Dalili hazikuwa nzuri kwa Leeds kabla ya mechi, kwani Whites hawajawahi kushinda mechi ya nyumbani ya Ligi Kuu dhidi ya timu iliyoanza siku ikiwa kileleni mwa msimamo, lakini mashabiki wa Elland Road walitarajia kuona mapambano zaidi kutoka kwa timu yao.
Hata hivyo, isipokuwa dakika 15 za mwanzo na kipindi kifupi kabla ya bao la Gyokeres, kikosi cha Daniel Farke kilizidiwa kila upande na bado wako hatarini kushuka daraja. Matokeo ya mechi za Jumamosi, Brighton ilifungana 1-1 na Everton, wakati Wolves ilikubali kichapo cha mabao 2-0 nyumbani kutoka kwa Bournemouth.
TAKWIMU ZA MECHI LEEDS vs ARSENAL
Umiliki wa mpira: Leeds 49% – 51% Arsenal
Mashuti: Leeds 3 – 14 Arsenal
Mashuti yaliyolenga lango: Leeds 1 – 8 Arsenal
Kona: Leeds 4 – 12 Arsenal
Faulo: Leeds 10 – 7 Arsenal