Arsenal mzuka, bei ya Sesko yashuka

Muktasari:
- Arsenal bado haijasaini straika mpya kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, lakini imemfanya Sesko kuwa chaguo la kwanza kwenye mchakato huo wa usajili.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imepata mzuka kwenye mchakamchaka wa kumfukuzia straika Benjamin Sesko baada ya klabu ya RB Leipzig kuripotiwa kushusha bei.
Arsenal bado haijasaini straika mpya kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, lakini imemfanya Sesko kuwa chaguo la kwanza kwenye mchakato huo wa usajili.
Kocha Mikel Arteta anafahamu wazi kwamba anahitaji straika wa kiwango cha dunia ili kuboresha fowadi yake kuwa ya kibingwa baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu England kwa misimu mitatu mfululizo.
Mkurugenzi wa michezo wa Arsenal, Andrea Berta ndiye mtu mwenye majukumu ya kusaka straika wa maana, akiwaweka ubaoni Sesko na straika wa Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres.
Lakini, vitu vimekuwa kimya kwa siku za karibuni, jambo ambalo limekuwa likiwapa wasiwasi mashabiki, wakitaka kufahamu ni straika gani hasa atasajiliwa. Hata hivyo, uvumilifu wa Arsenal unaonekana kulipa baada ya gazeti la Bild kuripoti kwamba Leipzig imeamua kushusha bei anayouzwa mshambuliaji huyo.
Mwanzoni klabu hiyo ya Ujerumani ilikuwa inataka ada kati ya Euro 80 milioni na Euro 100 milioni kwenye mauzo ya Sesko. Hilo liliikata maini klabu hiyo ya Ligi Kuu England na kufikiria wabadala.
Lakini, sasa inaripotiwa bei ya mchezaji huyo imeshuka hadi Euro 70 milioni, huku straika huyo mkataba wake Leipzig ukifika tamati Juni 2029 na alifunga mabao 21 katika mechi 45 za michuano yote alizocheza msimu uliopita.
Arsenal kwa muda mrefu imekuwa ikimfukuzia straika Sesko na inaamini kuwa ni chaguo bora zaidi kuliko Gyokeres, hasa kwenye umri wa wachezaji hao wawili, huku wakiamini anatokea kwenye ligi yenye ushindani mkali kuliko Ureno alikotamba Gyokeres.