Arnold alikuwa na misuli iliyobeba pesa

CALIFORNIA, MAREKANI. ARNOLD Schwarzenegger ni moja ya majina makubwa kwenye tasnia ya filamu. Dunia inamtambua. Miaka ya 1970 hadi 1990 aliiteka dunia kwa filamu zake za mapambano, anzia ‘Hercules in New York’ ya mwaka 1970 ndiyo iliyomtambulisha kwenye tasnia hii.

Ana asili ya Austria aliyechukua uraia wa Marekani na tofauti na uigizaji pia ni mfanyabiashara, mtayarishaji filamu, mwanasiasa na kwenye michezo alikuwa ni mtunisha misuli.

Baada ya kutambuliwa na filamu hiyo ya kwanza, alishusha kazi nyingi zikiwamo zile pendwa kama Commando, Teminator zote, Predetor, True Lies, Eraser, Collateral Damage na nyingine nyingi.
Filamu ni moja ya mambo yaliyomwingizia pesa nyingi Schwarzenegger ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 76.

Kabla ya kuingia kwenye uigizaji, Schwarzenegger alikuwa ni bingwa wa kunyanyua vitu vizito na huko pia alitengeneza pesa ndefu.

Ni mchezo huo uliomfanya awe na mwili uliotumika kama dili kwa watayarishaji wa filamu kutamani kumtumia kwenye kazi zao na walifanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani filamu alizoigiza zilihusu mapigano na kutumia nguvu na kwa mwili aliokuwa nao kipindi hiko, alionyesha uhalisia kwenye filamu.
Mbali na kwamba kwa sasa amezeeka, lakini bado anaendelea kutengeneza pesa na katika historia ya maisha yake aliwahi kuwa Gavana wa Jimbo la Carlifonia, Marekani.

MAISHA NA PESA
Ukweli miaka ya 1980 na 90, kazi zake za filamu zilimwingizia pesa nyingi na hadi sasa ana utajiri wa Dola 450 milioni na kiasi kikubwa ni kutokana na filamu zake na alipata Dola 400 milioni kutokana na kazi zake.
Filamu yake iliyompa pesa nyingi ni ‘Twins’ ya mwaka 1988 na alipata Dola 40 milioni ingawa alipewa kutokana na mapato ya filamu hiyo akichukua asilimia 33 tu, huku filamu hiyo ikiingiza jumla ya Dola 215 milioni.


Aliendelea mkutengeneza pesa kutokana na filamu na ile ya The Terminator I aliingiza Dola 75,000, akapata Dola 2 milioni kwenye Commando, Dola 3.5 milioni kwenye filamu ya Predator kisha akakunja Dola 11 milioni katika muvi ya Total Recall, Dola 12 milioni kwenye Kindergarten Cop ambayo ni sawa na ile aliyoipata kwenye Terminator II kila neno alilozungumza alilipwa Dola 21,429.

Muvi nyingine kama True Lies, Junior, Last Action Hero alilipwa Dola 15 milioni kila moja na kwa upande wa Eraser, Jingle All The Way alipata Dola 25 milioni na muvi zote zilizobakia baada ya hapo kila moja alipata Dola 25 milioni, isipokuwa Terminator III na inakadiriwa alipata Dola 35 milioni.
Ukiondoa pesa hizo, Schwarzenegger pia anaingiza pesa kutokana na biashara zake na amewekeza kwenye mijengo na hoteli ambazo nyingi zipo huko Kusini mwa California, hoteli na mijengo hiyo inakadiriwa kuwa na thamani ya Dola 100 milioni.
Jamaa pia ni balozi wa kampuni mbalimbali kama Oak Production, Planet Hollywood na Dimensional Fund Advisor.
Kupitia cheo chake cha kuwa Gavana wa California kuanzia mwaka 2003 hadi 2011 alikuwa akipata Dola 60,000 kwa mwezi.


MIJENGO
Mwaka 2002, alitumia Dola 4.8 milioni kununua nyumba yenye upana wa futi 14,500 ambayo ndani yake ina kiwanja cha tenisi, bwawa la kuogelea, ukumbi wa sinema, sehemu ya kufanyia mazoezi na hata sehemu kwa ajili ya vinywaj.


NDINGA
Kreisel Hummer electric - Pauni 100,000
Bentley Continental GT Convertible - Pauni 220,000
Dodge Challenger SRT8 - Pauni 50,000
Dodge Challenger SRT8 - Pauni 50,000
Tesla Roadster  -Pauni 150,000

MSAADA KWA JAMII
Kwa mujibu wa mtandao wa Imdb, Arnold alikuwa akitoa mshahara wake wote wa ugavana kwenda kusaidia jamii.
Pia akiwa katika nafasi hiyo alikuwa akitoa misaada ya kupambana na magonjwa mbalimbali kama Ukimwi, Kisukari na pia amekuwa mdau wa kusaidia watoto walemavu.


MAISHA BINAFSI
Kuanzia mwaka 1986 hadi 2022 alikuwa kwenye mahusiano na Maria Shriver, mpwa wa aliyekuwa Rais wa Marekani, John F. Kennedy na walipata watoto wanne.
Ndoa yao iliingia dosari mwaka 2011 baada ya kubainika Schwarzenegger alimsaliti kwa mfanyakazi wao wa ndani na amezaa naye mtoto ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 14.
Maria alidai talaka ambayo ilichukua zaidi ya miaka sita kutoka na inaelezwa Schwarzenegger alipoteza takribani Dola 200 milioni kwa kumlipa mkewe huyo baada ya talaka.