Antony ahama na kijiji Real Betis
Muktasari:
- Real Madrid ilikubali kichapo cha mabao 2-1 uwanjani Benito Villamarin, hivyo kupoteza fursa ya kupanda kileleni mwa msimamo wa La Liga.
MADRID, HISPANIA: MASHABIKI wa Real Madrid wametamba kwamba mzuka wa winga wa Kibrazili, Antony umechangia timu hiyo kuvuruga mipango ya Real Madrid katika mbio za ubingwa wa La Liga msimu huu.
Real Madrid ilikubali kichapo cha mabao 2-1 uwanjani Benito Villamarin, hivyo kupoteza fursa ya kupanda kileleni mwa msimamo wa La Liga.
Antony, 25, alicheza kwa dakika zote 90 akiwa na kikosi cha Betis akiendelea kuwasha moto kwa kucheza kwa kiwango bora sana ndani ya uwanja. Winga huyo wa Manchester United hakufunga wala kuasisti, lakini aliendelea kuwasumbua mabeki wa Real Madrid kwa muda wote na kufanya Betis ishinde.
Brahim Diaz aliifungia Real Madrid bao la utangulizi dakika ya 10 tu mchezo, lakini wachezaji wenzake Antony, Johnny Cardoso na Isco, ambaye aliwahi kuichezea Real Madrid, walipindua meza kufanya matokeo yasomeke 2-1. Cardoso alifunga bao la kusawazisha kabla ya Isco kufunga la ushindi kwa penalti baada ya beki wa kati wa Los Blancos, Antonio Rudiger mwangusha ndani ya boksi Jesus Rodriguez.
Lakini, mashabiki katika mitandao ya kijamii wanaamini hilo limewezekana kutokana na mzuka wa Antony.
Shabiki mmoja aliposti: “Mzuka wa Antony umetosha kuleta ushindi.”
Mwingine aliandika: “Antony madhara yake kwenye timu ni makubwa.”
Na shabiki wa tatu aliandika: “Antony na mzuka wake ndio huo.”
Shabiki wa nne alisema: “Tumsifu bwana Antony.”
Kuna shabiki alisema: “Hebu tuwacheke Man United kwa kumtoa kwa mkopo Antony.”
Katika mechi hiyo, takwimu za Antony zinasoma aligusa mpira mara 64, pasi sahihi 35 kati ya 38 alizopiga, amepiga shuti moja na krosi tatu.
Matokeo hayo yaliifanya Real Madrid kubaki na pointi 54.