Antoine Griezmann kumfuata Messi MLS
Muktasari:
- Messi na Griezmann walicheza pamoja Barcelona kwa misimu miwili kuanzia Julai 2019 hadi Agosti 2021, na katika kipindi hicho wachezaji hao walikipiga uwanjani katika La Liga, Copa del Rey na Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya Messi kuhamia PSG na Griezmann kurudi Atletico.
ORLANDO, MAREKANI: MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Ufaransa, Antoine Griezmann anatarajiwa kuwa “mpinzani” wa Lionel Messi tena katika Ligi kuu Marekani (Major League Soccer - MLS), jambo linalofufua kumbukumbu za uhusiano uliokuwa na sintofahamu walipokuwa pamoja Barcelona.
Messi na Griezmann walicheza pamoja Barcelona kwa misimu miwili kuanzia Julai 2019 hadi Agosti 2021, na katika kipindi hicho wachezaji hao walikipiga uwanjani katika La Liga, Copa del Rey na Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya Messi kuhamia PSG na Griezmann kurudi Atletico.
Griezmann anayeichezea Atletico Madrid ya Hispania anatarajiwa kujiunga na Orlando City, wapinzani wakubwa wa Inter Miami, timu anayochezea Messi na Mfaransa huyo ameripotiwa kusafiri kwenda Marekani kukamilisha makubaliano yake, ingawa atamaliza kwanza msimu akiwa chini ya kocha Diego Simeone.
Mchezaji huyo aliwahi kusema kucheza MLS ni ndoto yake ya kumalizia soka: “Ni lengo langu. Nataka kumalizia kazi yangu huko, kufurahia ligi na pia michezo mingine ya Marekani ambayo ninaipenda.”
Pia alimpongeza Messi kwa mchango wake mkubwa katika ligi hiyo akisema: “Leo (Messi) ndiye bora zaidi katika historia. Anajaza viwanja, anafunga mabao mengi na tangu afike (Marekani) timu yake inashinda. Ni mchezaji wa ajabu.”
Uhusiano wa Messi na Griezmann ulizungumzwa sana walipokuwa Barcelona na Griezmann alikiri siku ya kwanza alipojiunga nyota huyo alimwambia alikerwa na uamuzi wake wa awali wa kukataa kujiunga na timu hiyo.
Messi aliwahi kusema: “(Griezmann) ni mmoja wa wachezaji bora kwa sasa. Tunafurahi kuwa naye Barcelona.”
Hata hivyo, wawili hao walikiri kuwa hawakuwa wakizungumza sana, jambo lililofanya uhusiano baina yao uonekane wa kawaida na siyo wa karibu. Mvutano mkubwa ulizuka baada ya kauli za aliyekuwa wakala wa Griezmann, Eric Olhats, aliyedai kuwa Messi ana ushawishi mkubwa sana klabuni na kutofurahia ujio wa Griezmann.
Kauli hiyo ilimuweka Griezmann kwenye wakati mgumu, lakini alikanusha haraka na kusisitiza kuwa hana uhusiano na wakala huyo tena na kwamba anamheshimu sana Messi akiendelea kujifunza kutoka kwake.
Vyombo vya habari ikiwamo L’Equipe viliripoti kuwa straika mwingine wa klabu hiyo wakati huo, Luis Suarez alijaribu kuboresha uhusiano kati ya wawili hao. Hata hivyo, hakufanikiwa. Suarez alihamia Atletico Madrid wakati Griezmann naye alirudi huko kwa mkopo 2021. Messi, kwa upande wake alijiunga na PSG.
Wawili hao walikutana tena katika fainali ya Kombe la Dunia 2022 Qatar na Argentina ya Messi ilishinda huku Griezmann akikosolewa kwa kiwango duni akiichezea Ufaransa.
Kwa sasa macho yataelekezwa MLS kuona kama Griezmann ataipa changamoto Inter Miami ya Messi huko Florida.
Griezmann aliwahi pia kusema: “Nilipokuwa Barcelona, vyombo vya habari vilikuwa vinaandika kila siku kwamba Messi hakuwa na furaha nami. Lakini, Messi aliniambia, ‘usijali hayo, ni mambo ya vyombo vya habari’. Uwanjani alinipa nafasi ya kupiga penalti na kushangilia mabao yangu kama yake.”