Amorim akutana na mabosi Man United

Muktasari:
- Mreno huyo alishuhudia kikosi chake kikichapwa 1-0 na Tottenham katika fainali hiyo iliyofanyika Bilbao, Hispania, Jumatano iliyopita.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA Ruben Amorim alilazimika kusafiri hadi Monaco kwenda kuzungumza na mabosi wa Manchester United saa chache baada ya kichapo fainali ya Europa League.
Mreno huyo alishuhudia kikosi chake kikichapwa 1-0 na Tottenham katika fainali hiyo iliyofanyika Bilbao, Hispania, Jumatano iliyopita.
Kikosi cha Amorim kimekuwa na msimu mbaya sana kwenye Ligi Kuu England, kikipoteza mechi 18 na kumaliza msimu kwenye nafasi ya 15 katika msimamo. Amorim, 40, alijiunga na Man United, Novemba mwaka jana kwenda kuchukua mikoba ya Erik ten Hag baada ya kufunguliwa mlango wa kutokea.
Ripoti zinafichua kwamba kocha huyo alitakiwa kwenye kikosi cha mabosi wa Man United huko Monaco kwenye kikao cha mwezi, ambapo mabosi wa timu hiyo wamekuwa wakikutana kila mwezi.
Kocha amekuwa hahudhurii kikao hicho, lakini kwa safari hii baada ya timu kupoteza fainali, alihitajika kuhudhuria.
Baada ya kikao, Amorim alirejea Manchester na kuwaambia wachezaji wake kwamba ataendelea kubaki kwenye kikosi hicho hadi msimu ujao.
Kabla ya fainali hiyo ya Bilabo, Amorim alikuwa anafikiria kuachana na miamba hiyo ya Old Trafford kama bodi na mashabiki watamwona kama si mtu sahihi kwenye timu.
Lakini, sasa ametuliza akili yake na kujenga hatima mpya ya klabu hiyo. Na katika siku ya mwisho ya msimu wa Ligi Kuu England, wakati Man United ilipoichapa Aston Villa 2-0 uwanjani Old Trafford, kocha Amorim alichukua kipaza saini na kuwaomba radhi mashabiki kwa msimu mbaya, kisha akawaambia “nyakati njema zinakuja.”