Alonso kupiga bei kibao Real Madrid
Muktasari:
- Hatima ya Rodrygo kwenye kikosi cha Los Blancos imekuwa katika mashaka makubwa, huku mkali huyo wa Kibrazili akihusishwa na timu za Arsenal na Paris Saint-Germain.
MADRID, HISPANIA: REAL Madrid imeripotiwa kuanza kupokea ofa kwa ajili ya mastaa wake watatu, Rodrygo, Brahim Diaz na Dani Ceballos ambao imepanga kuwapiga bei kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi baada ya kutokuwapo kwenye mpango wa kocha mpya, Xabi Alonso.
Hatima ya Rodrygo kwenye kikosi cha Los Blancos imekuwa katika mashaka makubwa, huku mkali huyo wa Kibrazili akihusishwa na timu za Arsenal na Paris Saint-Germain.
Kwa mujibu wa Fichajes, Diaz na Ceballos nao wanaweza kuungana na Rodrygo kwenye orodha ya wachezaji wanaoweza kuachana na maisha ya Bernabeu kwenye dirisha hili, kwa sababu kocha Alonso hana hesabu za kuwatumia kwenye msimu wa 2025-26.
Ripoti zinafichua wachezaji hao walishindwa kufanya vizuri kwenye fainali za Kombe la Dunia la Klabu, ambako kocha Alonso alikuwa na nafasi ya kuwaangalia wachezaji wake ili kujua nani wa kubaki naye kwenye kikosi kwa ajili ya msimu ujao.
Rodrygo alicheza dakika 92 tu kwenye fainali hizo, ambapo kocha Alonso anataka kuwa na safu mpya ya washambuliaji kwenye kikosi chake.
Kiungo Ceballos alicheza mechi nne kwenye Kombe la Dunia la Klabu, lakini hesabu yake ni dakika 70 tu ndizo alizokuwa uwanjani kwa sababu kuna wachezaji wengine waliokuwa wakipewa nafasi zaidi. Mkataba wa Ceballos utafika tamati Juni 2027, huku Diaz - ambaye pia hakuwa na wakati mzuri sana kwenye kikosi hicho wakati wa fainali za Kombe la Dunia la Klabu, akicheza dakika 103, amekuwa kwenye rada za Bayern Munich wakihitaji huduma yake.