Alisson aondoka kambini Liverpool
Muktasari:
- Mbrazili huyo hakushiriki mazoezi ya Jumanne yaliyofanyika JFA Dream Field, Tokyo kutokana na sababu hizo. Baadaye ilielezwa Alisson alipewa ruhusu na klabu yake ya Liverpool kuondoka Japan haraka.
LIVERPOOL, ENGLAND: KIPA wa Liverpool, Alisson Becker ameripotiwa kuondoka kwenye kambi ya timu hiyo katika ziara yao ya pre-season huko Asia kutokana na kuwa na matatizo binafsi.
Mbrazili huyo hakushiriki mazoezi ya Jumanne yaliyofanyika JFA Dream Field, Tokyo kutokana na sababu hizo. Baadaye ilielezwa Alisson alipewa ruhusu na klabu yake ya Liverpool kuondoka Japan haraka.
Hiyo ina maana hatakuwapo uwanjani kwenye mechi wa Jumatano dhidi ya Yokohama F Marinos kwenye Uwanja wa Nissan.
Alisson, 32, atajiunga na kikosi hicho cha Arne Slot kitakaporudi Uingereza, kwa mujibu wa gazeti la The Athletic.
Kipa mpya aliyejiunga na Liverpool kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, Giorgi Mamardashvili, aliyenaswa kutoka Valencia, anatarajia kuanzishwa kwenye mechi hiyo ya Jumatano dhidi ya klabu hiyo inayocheza J1 League.
Kocha Slot bado ana makipa wengi wa kuziba nafasi akiwamo Freddie Woodman, Armin Pecsi na Kornel Misciur, ambao wapo pia kwenye ziara. Alisson ni mchezaji wa tatu kuondoka kwenye kambi ya Liverpool huko Asia.
Luis Diaz, 28, aliondoka kwenda kukamilisha uhamisho wake wa Pauni 65.5 milioni kujiunga na mabingwa wa Bundesliga, Bayern Munich.
Na beki Joe Gomez, naye aliondoka kwenye timu hiyo baada ya kupata maumivu ya mshipa wa mguu, hivyo alihitaji kufanyiwa uchunguzi zaidi wa vipimo huko Merseyside. Liverpool iliwasili Tokyo, Jumapili baada ya kichapo cha mabao 4-2 kutoka kwa AC Milan katika mechi iliyofanyika Hong Kong.
Alisson anaweza kujiunga na wenzake wakati Liverpool itapocheza na Athletic Bilbao uwanjani Anfield, Agosti 4, kabla ya siku sita baadaye, miamba hiyo kukipiga na Crystal Palace kwenye Ngao ya Jamii, Agosti 10.
Liverpool itafungua pazia la Ligi Kuu England kwa kuwakabili Bournemouth uwanjani Anfield, Agosti 15.