Algeria kujitoa CAF

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa ripoti zilizochapishwa katika tovuti za Beinsports na ghanasportscenter.com ni kwamba Algeria inaamini uamuzi mwingi wa CAF una upendeleo na kuionea.

SHIRIKISHO la Soka la Algeria (FAF) limepanga kujiondoa uanachama katika Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na kujisajili katika Shirikisho la Soka la Asia (AFC), kwa kile linachoeleza kwamba haliwatendei haki.

Kwa mujibu wa ripoti zilizochapishwa katika tovuti za Beinsports na ghanasportscenter.com ni kwamba Algeria inaamini uamuzi mwingi wa CAF una upendeleo na kuionea.

Algeria imekuwa mwanachama wa CAF tangu Oktoba 1962 ikiwa ni karibu miaka 61 kiasi cha kuwa moja kati ya wanachama wakongwe wa shirikisho hilo.

Mashabiki wengi nchini humo wanaamini uamuzi wa Algeria kujiondoa CAF umechagizwa na kitendo cha RS Berkane kupewa mabao sita mbele ya USM Alger baada ya kutokea mzozo baina ya timu hizo mbili kiasi cha kusababisha mechi za nusu fainali mkondo wa kwanza na wa pili katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu zisichezwe.

Katika miaka 61 iliyodumu ndani ya CAF, Algeria imefanikiwa kushinda mataji mawili ya Afcon kupitia timu ya taifa, matano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika mara moja yaliyobebwa na klabu za nchi hiyo.