AJ amtaka Tyson, Usyk ni Dubois

HATIMAYE Anthony Joshua ‘AJ’ alijirudisha kwenye ubabe wake wa ushindi kwa kumchapa mpinzani wake, Jermaine Franklin wikiendi iliyopita, ukumbini 02 Arena mjini London, kwa kura za majaji wote watatu (UD).

Ushindi huo ndio uliompa nguvu mpya AJ ya kutangaza hadharani anamhitaji Mwingereza mwenzake, Tyson Fury ili wapambane ulingoni kukata kiu ya mashabiki wao waliowakosa mwaka 2021 kama ilivyowahi kukubaliwa baina yao.

Tofauti na ilivyokuwa wakati ule AJ alipokuwa na mikanda mitatu ya uzito wa juu, safari hii kama pambano litapangwa, watashindania mkanda wa WBC alionao Fury ambaye pambano lake dhidi ya Oleksandr Usyk halijathibitika kuwepo.

Kuvunjika kwa makubaliano ya pambano la Tyson na Usyk, limemfanya promota Alex Krassyuk wa Usyk kufikiria uwezekano wa kujadili mpango wa pambano dhidi ya Daniel Dubois ili kutetea mkanda wake wa WBA.