Aguero aitaja Man City, Foden
Muktasari:
- Kikosi hicho cha Kocha Pep Guardiola kilifanya vibaya kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, ilipomaliza nje ya Top Two.
MANCHESTER, ENGLAND: STAA wa zamani wa Manchester City, Sergio Aguero anaamini timu hiyo itanyakua ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu na kiungo mshambuliaji Phil Foden atabeba tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka.
Kikosi hicho cha Kocha Pep Guardiola kilifanya vibaya kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, ilipomaliza nje ya Top Two.
Dirisha hili la majira ya kiangazi imefanya maboresho kwa kumsajili Rayan Cherki, ambaye aliyekuja kuchukua buti za Kevin De Bruyne.
Aguero anaamini sasa timu yake itarudi matawi ya juu kwenye ligi msimu huu baada ya kushinda mara sita katika kipindi cha misimu saba kabla ya Liverpool haijabeba msimu uliopita.
Staa Aguero anaamini Liverpool itakuwapo kwenye Top Four, huku akizipa nafasi pia Arsenal na Chelsea zitakata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Gwiji huyo wa Man City anaamini Foden atakuwa mtu muhimu kwenye kikosi cha Etihad msimu huu. Kiungo huyo mchezeshaji hakuwa na wakati mzuri msimu uliopita, lakini hilo halina maana ni mchezaji wa kawaida.
Miaka miwili iliyopita, Foden alipaisha Man City na kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England na hilo ndilo linalomfanya Aguero kuamini atarudi tena kwenye viwango hivyo, lakini kwenye tuzo ya mchezaji bora wa mwaka atakuwa na wakati mgumu wa kushindana na mkali wa Chelsea, Cole Palmer.
Aguero: “Ningependa Foden ashinde tena tuzo ya mchezaji bora wa mwaka. Nimemtaja Phil, pia kuna (Alexis) Mac Allister, Enzo Fernandez, Cole Palmer na Declan Rice. Wote hao wanaweza kuonyesha viwango bora.”
Kwenye ishu ya mabao, Aguero anaamini Erling Haaland ataendelea kuwa tishio licha ya Ligi Kuu England msimu huu kuwapo na mastraika wengine matata akiwamo Viktor Gyokeres wa Arsenal na Benjamin Sesko wa Manchester United.