Afcon ilivyoondoka na utamu wake

Wenyeji wa Fainali za Afcon 2023, Ivory Coast wametwaa taji la michuano hiyo mikubwa Afrika baada ya kuifunga Nigeria mabao 2-1 kwenye mchezo wa fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Alassane Ouattara jana usiku.

Mabao mawili ya Frank Cassie na Sebastien Haller yaliiwezesha Tembo hao kutwaa ubingwa huo mbele ya Tai ikiwa ni baada ya miaka tisa tangu mara ya mwisho ibebe mwaka 2015.

Mchezo huo ulishuhudiwa na Rais wa nchi hiyo, Alassane Ouattara; Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), Gianni Infantino na wa Shirikisho la Soka Afrika, Patrice Motsepe; Mkurugenzi wa Ufundi wa Fifa na Kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger na magwiji wa zamani wa soka Nwanko Kanu wa Nigeria, Didier Drogba na Solomon Kalou wa Ivory Coast pamoja na wengine.

Ilikuwa ni burudani ya aina yake kwa timu zote kushambuliana kwa zamu huku bahati ikienda kwa Tembo wa Ivory Coast ambao wamebeba taji hilo kwenye ardhi ya nyumbani na kuibua shangwe kwa mashabiki wao waliokuwa wengi uwanjani.

Fainali hizi zilifunguliwa na kufungwa katika Uwanja wa Alassane Ouattara na nyota wa Ivory Coast waliungana na rais wa nchi hiyo, Ouattara kufurahia ubingwa huo. Hizi hapa takwimu na mambo mbalimbali yaliyoibua furaha.


MOROCCO YAKABIDHIWA BENDERA
Morocco ambao ndiyo itakayoandaa fainali zijazo za Afcon 2025, imekabidhiwa Bendera ikiwa ni kudhihirisha rasmi michuano hiyo ya 34 itafanyika kwenye ardhi ya nchi hiyo.
Morocco ambayo kwenye fainali za 2023 ilitolewa katika hatua ya 16 bora na Afrika Kusini kwa mabao 2-0, itaandaa fainali hizo zilizopangwa kuanzia Juni hadi Julai, mwaka kesho.


KIPA NA TIMU BORA
Kipa na nahodha wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Ronwen Williams anayekipiga katika timu ya Mamelodi Sundowns ya nchini humo ametwaa tuzo ya kipa bora wa Afcon 2023.

Ronwen alipata sifa baada ya kuonyesha kiwango bora kwenye fainali hizo akimpiku kipa wa Nigeria, Stanley Nwabili aliyepewa nafasi kubwa baada ya kuifikisha timu yake fainali huku akiwa amefungwa mechi machache kabla ya kufungwa mabao mawili katika mchezo wa mwisho dhidi ya Ivory Coast.

Kipa huyo aliokoa pia penalti kwenye robo fainali za michuano hiyo dhidi ya Cape Verde katika hatua ya mikwaju mitano ya penalti na kuipeleka timu hiyo nusu fainali.

Afrika kusini licha ya kuwa mshindi wa tatu kwenye michuano hiyo pia imechukua tuzo ya timu yenye nidhamu na kuondoka na medali ya shaba.

KIATU CHA DHAHABU
Nyota wa timu ya Taifa ya Equatorial Guinea, Emilio Nsue ametwaa kiatu cha dhahabu cha mfungaji bora baada ya kuibuka kinara akitupia mabao matano kwenye fainali hizo.

Nsue 34 anayekipiga katika timu ya Intercity nayoshiriki Ligi Daraja la Tatu Hispania, ameifungia timu ya taifa lake mabao matano, akifanya hivyo kwenye mechi mbili dhidi ya Guinea Bissau matatu (hat trick) katika ushindi wa mabao 4-1 na mawili dhidi ya Ivory Coast katika ushindi wa mabao 4-0 yote kwenye hatua ya makundi katika kundi A lililokuwa pia na timu ya Nigeria na kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu vya Afcon.

Rekodi ya ufungaji na kiatu cha dhahabu fainali za Afcon zilizopita 2021 zilizofanyika Cameroon, inashikiliwa na Mcameroon Vicent Aboubakar aliyemaliza akiwa na mabao manane.

Rekodi ya muda wote ya ufungaji bora wa mabao fainali za Afcon inashikiliwa na Samuel Eto'o aliyefunga 18 katika mechi 29.

MCHEZAJI BORA NA SAMATTA
Beki wa kati wa Nigeria, William Troost-Ekong ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa Afcon.

Kona ya Ademola Lookman iliyopigwa kwa kichwa na kiungo wa Ivory Coast, Jean Michael Seri kwenye lango kwa karibu, na Troost-Ekong akaruka juu ya Serge Aurier na kuuongoza mpira nyuma ya goli na kumpita kipa wa Tembo, Yahia Fofana.

Beki huyo anayekipiga katika klabu ya PAOK inayoshiriki Ligi Kuu ya Ugiriki anacheza na Mtanzania Mbwana Samatta.