Mbappe anakuja Man City kivyovyote

MANCHESTER, ENGLAND. UNAAMBIWA huko jijini Manchester, mmiliki wa Man City, Sheikh Mansour, ameamua kula kiapo cha kumshusha staa wa PSG na Ufaransa, Kylian Mbappe katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi kwa gharama yoyote.
Baada ya kuikosa saini ya Cristiano Ronaldo katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi tajiri huyo ameamua kuwekeza muda na pesa kwa Mbappe ili kuhakikisha anaipata huduma yake.
Hiyo ni kati ya habari mbaya kwa mabosi wa Real Madrid ambao walikuwa na uhakika wa asilimia kubwa za kuipata saini ya staa huyo mwisho wa msimu.
Madrid ilijaribu kupambana sana katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi kwa kuwasilisha ofa mara mbili lakini zote zilikataliwa na mabosi wa PSG wanaoamini staa huyo anaweza kukubali kuongeza mkataba mpya wakati wowote.
Man City imekuwa ikitafuta straika kwa muda mrefu na katika dirisha lililopita ilihitaji kumsajili staa wa Tottenham, Harry Kane lakini dau lililowekwa na Spurs lilikuwa kikwazo.
Wakati Madrid ikijipanga kumsajili Mbappe mwisho wa msimu akiwa mchezaji huru, Man City inataka kumaliza shughuli katika dirisha lijalo la majira ya baridi.
Mabingwa hao watetezi wamekuwa wakihaha kutafuta mbadala wa Sergio Aguero.