Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yondani: Beki wa kati asiye na mpinzani Ligi Kuu Bara

Kuzaliwa: Oktoba 9, 1985,

Mahali: Mwanza

Nafasi: Beki wa kati

Klabu: Toto Africa 2004-2006,Simba 2006-2012,Yanga 2012-

Jezi: Namba 5

Taifa: Tanzania

 

 

Muktasari:

  • Ana umbo la kawaida, lakini sifa yake kubwa ni kucheza mipira ya juu kwa kichwa, anatumia akili kwenye kukaba, ni mwiba wa kuogopwa na mastraika wakorofi.

NANI asiyefahamu makali ya Kelvin Patrick Yondani ‘Vidic’ wa Yanga anapokuwa kwenye himaya yake ya ulinzi ambapo  sasa anahesabika kuwa ndiye beki bora wa kati Tanzania.

Uimara wa Yondani ndiyo umemfanya apewe jina la Vidic wakimfananisha na beki wa Manchester United, Nemanja Vidic na yeye ndiye beki anayempenda.

Yondani ameufanya ukuta wa Yanga kusimama imara hadi sasa akishirikiana na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na msimu uliopita walitwaa taji la Ligi Kuu Bara na yeye akatangazwa mchezaji bora wa mwaka.

Ana umbo la kawaida, lakini sifa yake kubwa ni kucheza mipira ya juu kwa kichwa, anatumia akili kwenye kukaba, ni mwiba wa kuogopwa na mastraika wakorofi.

Yondani anasema siri ya yote hayo ni mazoezi, kufuata maelekezo ya kocha na ushirikiano wake na wachezaji wenzake kikosini.

“Kila kitu ni kujituma, nashukuru Mungu kwa yote, yeye ndiye kila kitu, ndiye aliyenijalia yote,”anasema.

Kikosi cha Yanga kwa sasa hasa safu ya beki wa kati ina ushindani ingawa Kocha Mkuu, Ernest Brandts ameendelea kuwaamini, Yondani na Cannavaro. Wapo wengine, Rajab Zahir, Ibrahim Job, Issa Ngao na Mbuyu Twite anayetumika kama beki wa kulia.

Yondani anasema: “Mafanikio yoyote lazima ukutane na changamoto, ndipo utajua kipimo cha nguvu yako.”

“Kweli katika nafasi ya beki wa kati tupo wengi, lakini ukweli utabaki pale pale anayejua ndiye atakayepata nafasi ya kucheza,”anaeleza Yondani.

“Ushindani unakufanya mchezaji ujipange na kutobweteka, unapokosa mshindani unabweteka na kufikiri nitapangwa tu. Lakini ushindani unakufanya ujitambue na kujipanga uwe vizuri kila siku kwani ukilala kidogo tu, mwana si wako tena.”

Kuhusu uchezaji bora wa ligi msimu huu baada ya kupata msimu uliopita, Yondani anasema: “Ndiyo tuko kwenye ngoma tunacheza, ligi inaendelea lakini mawazo yangu ni kujituma kuipa mafanikio Yanga.”

“Nitajitahidi kadri niwezavyo tufanikiwe na mambo mengine ya uchezaji bora, huwa yanafuata tu, ni mipango ya Mungu.”

Yondani ameenda mbali na kuzungumzia kombinesheni kikosini hapo kuwa anapocheza na yeyote anajisikia amani na huru zaidi.

“Anayejua anajua tu, sichagui wa kucheza naye, yeyote niko tayari kucheza naye,” anaeleza Yondani. 

Akizungumzia ligi msimu huu, Yondani anasema: “Ligi ni ngumu kila timu ipo vizuri na hakuna kibonde  kila unapogusa ni moto tu.”

“Na ngumu zaidi pale mnapotoka kucheza mechi za nje mnakutana na uwanja mpya, mazingira mapya na changamoto nyingine kama waamuzi na mashabiki.Yondani pia alizungumzia mechi ya  watani wa jadi linalowakutanisha wao na Simba Jumapili anasema: “Simba ni timu kubwa na nzuri, wamesajili wachezaji wengi vijana ni wazuri, wanajituma ingawa tatizo ni  uzoefu.”

“Kikosi chetu hakijabadilika sana, sehemu kubwa ni walewale, lakini  tutakapokutana kama ujuavyo mechi ya Simba na Yanga huwa haitabiriki.

“Siku zote huwa ni ngumu, unachotarajia kinaweza kisifikie ingawa, Simba wataendelea kuwa wateja wetu tu na mambo yote ni Oktoba 20,” anaeleza kwa kujiamini.

Mafanikio kwenye soka

Yondani anasema, anashukuru soka kwani ndiyo inaendesha maisha yake ya kila siku.

“Nimefanikiwa kujenga nyumba mbili, nina biashara zangu lakini pia sipigwi na jua, nina usafiri wangu (gari),” anasema katika maisha yake siku aliyofurahi kuliko zote ni pale alipopata mtoto mara ya kwanza (anaitwa Patrick).

“Nilifurahi sana kwa sababu nimepata chata, wapo matajiri na pesa zao lakini tatizo ni watoto,” anaeleza Yondani. Akizungumzia huzuni, Yondani anasema hajawahi kuwa katika kipindi kigumu matukio yoyote anayokutana nayo anayachukulia kama changamoto.

Sakata la usajili Simba na Yanga

Msimu uliopita, Yondani alikuwa kwenye wakati mgumu baada ya kudaiwa kusaini Simba na Yanga.

Simba walidai kumwongezea mkataba mpya na yeye akijua lakini akasajili kwa mara nyingine Yanga. TFF walipokaa na kuchunguza  walimuidhinisha  kuichezea Yanga.

Yondani anasema: “Ishu ile ni kama ilitengenezwa, ukweli kutoka moyoni sikusajili Simba.”

“Inawezekana wao wenyewe walipoona nimemalizana na Yanga waliamua kutengeneza ishu. “Sikupenda jambo lile lilinipa sifa mbaya kwenye jamii  na familia yangu.

Maisha nje ya soka

Yondani anasema, furaha yake kwenye chakula ni pale anapoandaliwa ugali na mlenda, mboga nyingine kama nyama, samaki au kuku ni ziada kwake.

Akizungumzia maisha yake nje ya soka. Yondani ambaye ni Mpogolo wa Mahenge, Morogoro aliyekulia Mwanza anasema: “Napenda kuwa nyumbani na familia yangu, kusikiliza muziki, kucheza na wanangu na kubadilishana mawazo.”

Yondani ameweka wazi kuwa, muziki anaopenda kuusikiliza ni hip-hop na nchini anawapenda Nako2nako, nje ni marehemu 2pac.

Historia

Yondani ni baba wa familia, mke wake anaitwa, Nasra Mussa. Ana watoto wawili wanaume, Patrick (5) na Brian mwenye miezi mitatu.

Yondani anasema: “Nataka watoto wangu wasome sana kwa sababu naamini elimu ndiyo kila kitu na mambo mengine yanafuata tu.”

Beki huyo alisoma Shule ya Msingi Kirumba na alimalizia Sekondari ya Lake, zote za Mwanza.

Alianza kucheza soka akiwa mdogo na alipomaliza masomo alisajiliwa na Toto ya Mwanza mwaka 2004, baadaye Simba hadi Yanga anayoichezea sasa.

Anasema kipaji chake ni urithi na alijikita kwenye soka kwa sababu alikuwa anavutiwa na kiwango cha baba yake mdogo, Mbuyi Yondani aliyekuwa mshambuliaji wa zamani wa Reli ya Morogoro na Simba.