KenGold yaikaushia mechi ya Simba

Muktasari:
- Timu hiyo iliyoshuka daraja sawa na Kagera Sugar baada ya kudumu msimu mmoja Ligi Kuu, imebakiwa na mechi mbili kumaliza Ligi ikiwa ni dhidi ya Simba na Namungo.
LICHA ya kubaki siku kama tano tu kabla ya kuvaana na Simba katika mechi ya kukamilishia ratiba baada ya kushuka mapema daraja, benchi la ufundi la Ken Gold limesema lipo njiapanda kutokana na timu hiyo kutokuwa kambini hadi sasa tofauti na walivyotaka ianze Juni 10.
Timu hiyo iliyoshuka daraja sawa na Kagera Sugar baada ya kudumu msimu mmoja Ligi Kuu, imebakiwa na mechi mbili kumaliza Ligi ikiwa ni dhidi ya Simba na Namungo.
KenGold ya wilayani Chunya, inatarajia kushuka uwanjani Juni 18, kuwakabili Wekundu hao waliopo nafasi ya pili kwa pointi 72, mechi ambayo itapigwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora.
Kapilima aliliambia Mwanaspoti hadi sasa timu haijaingia kambini na kila mmoja yupo nyumbani kwao na bado hawaelewi kinachoendelea kwa menejimenti.
Alisema awali taarifa za uongozi, timu ilipaswa kuingia kambini Juni 10, lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea na wanaendelea kusubiri hatma ya viongozi.
“Hatupo kambini, tuliambiwa tujiandae kuingia kambini Juni 10, lakini hadi leo ni kimya, kila mmoja yuko nyumbani kwake nami nipo Dar es Salaam, tunasubiri maelekezo ya viongozi,” alisema Kapilima.
Meneja wa timu hiyo, Charles Masai alisema pamoja na kuchelewa kuingia kambini, lakini matarajio yao ni wachezaji na benchi la ufundi kuanza kuingia kesho Ijumaa kujiandaa na mechi hiyo.
“Matarajio ni timu kuingia kambini kuanzia kesho, mechi yetu na Simba itapigwa Tabora kwa ratiba iliyopo hadi sasa, tunaamini maandalizi yataenda vizuri na kumaliza salama ligi,” amesema Masai ambaye alikuwa mchezaji wa timu hiyo.