Yanga yavuna Sh2.3 bilioni CAF

Yanga imejihakikishia kuvuna Dola 900,000 (zaidi ya Sh2.3 bilioni) kwa kutinga robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika jana Februari 23, 2024.

Mabingwa hao wa Tanzania wamefuzu hatua hiyo baada ya kuichapa CR Belouizdad mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Yanga ilifuta gundu la miaka 25 baada ya kutinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika na kuvuna Sh1.8 bilioni Septemba 30, 2023 ilipoing'oa Al Merrikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-0.

Endapo Yanga itafanikiwa kutinga nusu fainali ya mashindano hayo itavuna kitita cha Sh3.1 bilioni huku mshindi wa pili atapata Sh5.1 bilioni

Bingwa wa michuano hiyo atavuna zaidi ya Sh10.2 bilioni kiasi ambacho walipata Al Ahly msimu uliopita baada ya kuichapa Wydad 3-2 kwenye fainali hizo.

Yanga imeitangulia Simba kufuzu robo fainali na kuungana na bingwa mtetezi Al Ahly, Mamelodi Sundowns, TP Mazembe, Petro Luanda na Asec Mimosas.