Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga yatinga robo fainali Kagame

Donald Ngoma,  akimtoka mmoja wa mabeki wa KMKM katika harakati nyingine ya mchezo huo.  PICHA | SAID KHAMIS.

Muktasari:

  • Mabao ya kipindi cha pili yaliyotumwa kimiani na Malimi Busungu na jingine la kujifunga la beki wa KMKM, Ali Nassor, yalitosha kuihakikishia Yanga moja ya nafasi tatu za kundi la A ikiungana na  Al Khartoum ya Sudan na Gor Mahia ya Kenya zilizotangulia mapema katika hatua hiyo.

KIMEELEWEKA Jangwani baada ya Yanga jana Ijumaa kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMKM ya Zanzabir, na kutinga robo fainali ya michuano ya Kombe la Kagame huku ikipania ushindi zaidi kwenye mchezo ujao kesho Jumapili dhidi ya Al Khartoum.

Mabao ya kipindi cha pili yaliyotumwa kimiani na Malimi Busungu na jingine la kujifunga la beki wa KMKM, Ali Nassor, yalitosha kuihakikishia Yanga moja ya nafasi tatu za kundi la A ikiungana na  Al Khartoum ya Sudan na Gor Mahia ya Kenya zilizotangulia mapema katika hatua hiyo.

Pambano hilo lililochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, lilishuhudia timu hizo zikienda mapumziko bila ya bao  lolote licha ya kosakosa nyingi kwa kila timu.

Busungu aliyesajiliwa Yanga akitokea Mgambo JKT, alifunga bao ambalo kwake ni la tatu katika michuano hiyo. Alifanya hivyo katika dakika ya 56 kutokana na juhudi binafsi baada ya kupokea pasi na Geofrey Mwashiuya na kumzidi maarifa beki ya KMKM kabla ya kumtungua kipa Nassor Abdallah.

Mara baada ya Busungu kufunga bao hilo, Yanga iliendelea kufanya kosa kosa kupitia kwa mastraika wake wapya, Donald Ngoma aliyeisumbua sana ngome na KMKM akisaidiwa na Mwashiuya.

 Hata hivyo Busungu alipumzishwa na nafasi yake kuchukuliwa na Amissi Tambwe ambaye kukurukakara zake ziliisaidia Yanga kuandika bao la pili katika dakika ya 73 baada ya beki wa KMKM, Ali Nassor kujifunga katika harakati za kuokoa wakati akiwania mpira na Tambwe.

Kwa ushindi huo wa jana Yanga imefanikiwa kung’ang’ania nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi lao kwa kufikisha pointi 6 ikisaliwa na mechi moja dhidi ya vinara wa kundi hilo Al Khartoum ambayo mapema mchana ililazimishana sare ya bao 1-1 dhidi ya Gor Mahia.

Timu hizo mbili ambazo kama Yanga zimesaliwa na mechi moja moja kila moja ina pointi 7 na zitamaliza mechi zao siku ya Jumanne kwa Yanga kuumana na Al Khartoum na Gor Mahia kupepetana na Telecom ambayo ilishaaga mashindano hayo. KMKM imeshamaliza mechi zake ikiwa na pointi 3 ikimaliza katika nafasi ya nne.

Kwa ujumla pambano la jana lilikuwa kali na KMKM ilionyesha ilivyolipania pambano hilo kama ilivyokuwa katika mechi zao za awali, lakini katika kipindi cha pili baada ya kutunguliwa bao moja walilegea na kuipa nafasi Yanga kutawala, ingawa Jangwani itajilaumu kwa kushindwa kuibuka na ushindi mnono kutokana na washambuliaji wake kukosa umakini langoni mwa KMKM.

Baada ya mchezo Ngoma alitangazwa Mchezaji Bora wa Mechi.

Katika pambano la mapema mchana, Gor Mahia iling’ang’aniwa na Al Khartoum baada ya kutoka sare ya 1-1. Timu hizo zimetinga robo fainali zikiungana na APR ya Rwanda na Al Shandy za Kundi B na Azam ya Kundi C.

KMKM: Nassor Abdallah, Pandu Haji, Said Idrissa, Khamis Ali, Mussa Said, Ibrahim Khamis, Juma Mbwana, Tizo Chombo, Nassor Ali/Fakhi Sharif, Haji Simba na Mateo Simon.

YANGA: Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul/James Zuttah, Mwinyi Haji Mngwali, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite/Andrey Coutinho, Geofrey Mwashiuya, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Malimi Busungu/Amissi Tambwe na Deus Kaseke.