TFF yajibu tuhuma, yaithibitisha kuidai Yanga

Muktasari:
- Aprili 2, 2025, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lilitambulisha mkataba wa miaka mitatu iliosaini na Benki ya CRDB kwa ajili ya udhamini wa mashindano ya Kombe la Shirikisho la CRDB wenye thamani ya Sh3 bilioni.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepinga madai kuwa linadaiwa na Yanga, fedha za zawadi ya ubingwa ya mashindano ya Kombe la Shieikisho la CRDB msimu uliopita na badala yake limesema kuwa lenyewe ndio linaloidai klabu hiyo.
Taarifa iliyotolewa na TFF leo Juni 10, 2025 imeeleza kuwa kinyume na madai ya Yanga, klabu hiyo ndio inadaiwa na TFF.
“Tunapenda kuuthibitishia umma kuwa Benki ya CRDB ndiyo Mdhamini Mkuu wa mashindano ya Kombe la Shirikisho la TFF, na inatekeleza ipasavyo majukumu yake ya kimkataba.
“Kwa msimu wa 2023/2024 wa mashindano ya Kombe la Shirikisho la Benki ya CRDB (CRDB Bank Federation Cup), benki hiyo ililipa fedha zote za kimkataba Tsh. TSh 255,000,000/= (Milioni Mia Mbili na Hamsini na Tano) kwa ajili ya uendeshaji wa mashindano hayo.
“Tumemsikia Meneja Habari na Mawasiliano wa Young Africans SC kupitia vyombo vya habari akidai kuwa klabu yao inaida TFF Tsh. 200,000,000/= (Milioni Mia Mbili) ambayo ni zawadi ya ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Benki ya CRDB,” imefafanua taarifa ya TFF.
Taarifa hiyo ya TFF imefafanua kwamba Yanga ndio iliomba ikatwe fedha inazodaiwa na shirikisho hilo kupitia zawadi za ushindi za mashindano mbalimbali.
“Tunapenda kutoa ufafanuzi kuwa TFF ndiyo inayoidai klabu hiyo. Young Africans SC iliomba kwa barua fedha zao za zawadi katika mashindano mbalimbali zikatwe kulipia malipo wanayotakiwa kulipa kwa TFF ikiwemo ada za wachezaji wa kigeni.

“Hivyo, ili kutoendelea kusababisha sintofahamu kwa umma, tumeiandikia barua Young Africans kutuma kwetu mtaalamu wao wa fedha kesho saa 4 asubuhi kuhakiki deni la klabu hiyo akiwa na vielelezo vyote katika Ofisi za TFF.
“TFF itaendela kutekeleza wajibu wake wa kusimamia mpira wa miguu ikiwemo kulinda taswira za wadhamini wake,” imefafanua taarifa ya TFF.
Jana Jumatatu, Juni 9, 2025, Ałły Kamwe alisema kuwa Yanga inajiandaa kutocheza mechi ya Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB kwa vile haijapewa fedha zake za zawadi ya ubingwa za msimu uliopita.
“Taarifa hii iwafikie ofisi ya Katibu Mkuu wa TFF na wadhamini wa mashindano ya Kombe la Shirikisho la CRDB kuwa hatutacheza mchezo wa Fainali wa CRDB siku ya tarehe 28 mpaka tutakapolipwa hela yetu ya ubingwa kwa msimu uliopita. Tumevumilia dharau hizi kutoka kwa mamlaka za soka kwa muda mrefu sana. Sasa imefika mwisho. Hii ya Zanzibar pia hatutacheza,” alisema Ałły Kamwe.
Siku moja baada ya Yanga kutoa taarifa hiyo kuwa haitocheza mechi ya Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Singida Black Stars msimu huu hadi itakapolipwa fedha za zawadi za msimu uliopita, Benki ya CRDB inayodhamini mashindano leo ilitoa ufafanuzi na kujiweka kando na suala hilo.
Benki hiyo ilisema kuwa ilishafanya malipo ya fedha hizo kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
“Benki ya CRDB inapenda kutoa ufanunuzi wa madai yaliyotolewa na Msemaji wa Klabu ya Yanga katika mkutano wake na wanahabari uliofanyika tarehe 09 Juni 2025 katika Makao Makuu ya klabu hiyo.
“Katika mkutano huo, Msemaji wa Klabu hiyo alinukuliwa akitoa taarifa kwa Shirikisho la Mpira wa Migu Tanzania (TFF) na kwetu kama Mdhamini Mkuu wa mashindano ya Kombe la Shirikisho la Benki ya CRDB kuwa Klabu ya Yanga haitocheza fainali za mashindano hayo msimu huu kama hawatolipwa fedha za ubingwa wa msimu uliopita.
Tungependa kufahamisha umma na wadau wote wa soka kuwa Benki ya CRDB ni taasisi yenye kuzingatia weledi, kanuni na taratibu
na kwa msingi huo tayari Benki ilikwisha tekeleza kikamilifu wajibu wake wa kifedha kwa TFF kama sehemu ya makubaliano ya udhamini wa mashindano haya. Malipo yote ya msimu uliopita yalifanyika kwa TFF kwa mujibu wa mkataba baina ya Benki ya CRDB na TFF.
“Benki ya CRDB inatambua kuwa mbali na mchezo wa soka kuunganisha jamii yetu na kutoa burudani, lakini pia mchezo huu ni ajira kwa vijana wengi, hivyo dhamira yetu ni kuendelea kushirikiana na TFF, vilabu na wadau wengine katika kukuza mchezo huu kwa maslahi mapana ya Taifa letu,” imefafanua taarifa hiyo ya CRBD.