Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga yategwa dili la winga Mrundi

TBR Pict

Muktasari:

  • Yanga inayoongoza msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 73 baada ya kucheza mechi 28 ikiwa ni moja zaidi na ilizonazo Simba yenye 72 kwa idadi ya mechi kama hizo, itavaana na Prisons keshokutwa Jumatano kwenye Uwanja wa Sokoine, ikiwa ni kati ya mitatu iliyosaliwa nayo kufunga msimu.

KIKOSI cha Yanga kimesafiri kwenda Mbeya kuwahi pambano la Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons, huku mabosi wa klabu hiyo wakikuna vichwa kutoka na mtego waliowekewa juu ya kumnasa winga machachari Mnyarwanda anayekipiga Al Hilal ya Sudan.


Yanga inayoongoza msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 73 baada ya kucheza mechi 28 ikiwa ni moja zaidi na ilizonazo Simba yenye 72 kwa idadi ya mechi kama hizo, itavaana na Prisons keshokutwa Jumatano kwenye Uwanja wa Sokoine, ikiwa ni kati ya mitatu iliyosaliwa nayo kufunga msimu.


Lakini ikiwa inapambana kusaka ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo, mabosi wa Yanga walikuwa wakipiga hesabu kali za kumpata winga wa Al Hilal ya Sudan, Mrundi Jean Claude Girumugisha, lakini inaelezwa mabosi wa nyota huyo wameweka kiasi cha Sh3 bilioni kwa klabu yoyote inayomhitaji.

Nyota huyo aliyezaliwa Septemba 18, 2004, ameonyesha kiwango bora hadi sasa kutokana na uwezo  wa kucheza winga zote mbili uwanjani kwa ufasaha mkubwa kwa maana ya kulia na kushoto, jambo linaloziingiza vitani klabu kadhaa kumhitaji.

Hivi karibuni, Yanga iliripotiwa kuiwinda saini ya nyota huyo ingawa kwa sasa itakutana na ushindani kutokana na kiasi kikubwa cha fedha kilichowekwa ili kumpata kwa ajili ya kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji kikosini humo msimu ujao.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza sababu kubwa ya kiwango hicho kikubwa cha fedha ni kutokana na umri wake mdogo ambao unamruhusu kucheza kwa muda mrefu, huku ishu nyingine inayotajwa ni kutokana na kipaji alichokuwa nacho pia.

Mbali na hayo, ila mabosi wa Al Hilal wanaamini pia Yanga kwa sasa ina kiasi kikubwa cha fedha ilichoingiza, kutokana na mauzo ya aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa kikosi hicho, Stephane Aziz KI aliyejiunga na Wydad Casabalanca ya Morocco.

"Umri wake na mauzo ya Aziz KI ndio ambayo yamewafanya mabosi wa Al Hilal kuweka kiasi hicho kikubwa, wakitambua pia kwa sasa kuna dili linakaribia kukamilika la mshambuliaji, Clement Mzize kuuzwa Zamalek ya Misri," kilisema chanzo chetu.

Mtoa taarifa huyo aliyeomba jina lake kuhifadhiwa, alisema mauzo ya Aziz KI na yale ya Mzize yakikamilika ndiyo ambayo yanawawekea wakati mgumu, kwa sababu wachezaji wanaowahitaji wanapandishiwa bei wakiamini Yanga ina fedha za kutosha.

"Mauzo ya Aziz KI tayari na bado kuna hili la Mzize ambalo pia likikamilika Yanga itakuwa imeingiza kiasi kikubwa cha fedha, sasa kutokana na hilo hata wale tunaowaona ni wabadala wao thamani zao zimepanda sana," kilisema chanzo hicho.

Aziz KI aliyeuzwa Wydad Casablanca, inaelezwa Yanga imeingiza kiasi cha Dola 750,000 sawa na Sh2 bilioni, ambazo ni sawa na fedha ambazo mshambuliaji pia wa kikosi hicho, Clement Mzize amewekewa mezani na mabwenyenye wa Misri, Zamalek SC. 

Girumugisha alijiunga na Al Hilal ya Sudan Septemba 28, 2023, akitokea Magara Young Boys ya kwao Burundi, ambapo amekuwa na kiwango kizuri cha kuzivutia timu mbalimbali, huku msimu huu akifunga mabao 12 na kuasisiti 11 akiwa na kikosi hicho.

Pia, ameiwezesha timu hiyo chini ya Kocha, Florent Ibenge, iliyokuwa inashiriki Ligi Kuu ya Mauritania 'Ligue 1' msimu huu kutwaa ubingwa, baada ya kucheza mechi 30, ikishinda 20, sare saba na kupoteza mitatu, ikiongoza na pointi zake 67.

Al Hilal na Al Merrikh iliyomaliza nafasi ya sita na pointi 44, ziliomba kushiriki 'Ligue 1' kutokana na usalama mdogo huko kwao Sudan, ingawa awali Al Hilal iliomba kucheza Ligi Kuu Bara, kabla ya kupata muafaka na kuibukia Mauritania.