Yanga yasaka rekodi mpya Ethiopia

Muktasari:
- Kama hujui ni kwamba mabingwa wa Tanzania, Yanga wanakutana na mabingwa wenzao na wenyeji wa mchezo huo CBE SA katika mechi ya mkondo wa kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika ili kusaka tiketi ya kucheza makundi kwa msimu huu.
FANYA shughuli zako mapema kesho Jumamosi, kula chakula cha mchana kwa wakati kisha ikifika saa 9:00 mchana hakikisha macho yanakuwa mbele ya runinga kwani kuna mechi moja kubwa inapigwa makao makuu ya Afrika, jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Kama hujui ni kwamba mabingwa wa Tanzania, Yanga wanakutana na mabingwa wenzao na wenyeji wa mchezo huo CBE SA katika mechi ya mkondo wa kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika ili kusaka tiketi ya kucheza makundi kwa msimu huu.
Yanga itakuwa na dakika 90 ngumu za mechi hiyo mbele ya CBE inayotaka kuweka historia mpya msimu huu ambao ni wa kwanza kucheza mashindano hayo.
Wawakilishi hao wa Tanzania walitua kwa mafungu jana nchini humo baada ya wachezaji 14 kuwa kwenye majukumu ya kimataifa kwa timu za taifa, huku kila staa akiwasili kwa wakati huku wote wakiwa salama.
Akili ambayo waliitumia mabosi wa Yanga katika kufanikisha wachezaji hawaichelewi mechi hiyo ni kuhakikisha kila mchezaji aliyekwenda timu ya taifa anatumia ndege ya Shirika la Ethiopia mara baada ya kumaliza majukumu ya kimataifa basi ndege watakayopanda itawashusha Addis jambo luililofanikiwa.

DHIDI YA CBE
Yanga iko ugenini leo mechi ya mkondo wa awali wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya timu ya kitajiri ya CBE iliyokusanya wachezaji magalactico wa Ligi Kuu ya Ethiopia.
CBE inayomilikiwa na benki, ni timu iliyosajili kibabe na ni timu iliyofanya makubwa nchini Ethiopia baada ya kupanda daraja na moja kwa moja kwenda kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.
Ni timu chache sana ambazo zimewahi kupanda Ligi Kuu na kwenda moja kwa kutwaa ubingwa, CBE ni mojawapo na hili halikuja kwa bahati mbaya, bali linatokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na benki ya Biashara ya Ethiopia inayoimiliki timu hiyo.
Hii ni timu inayomiliki sana mpira, yaani boli linatembea kwelikweli --wachezaji wakiitendea haki staili ya uchezaji ya taifa hilo, mfano ukiwa ni mechi ya wiki iliyopita kati ya Taifa Stars ya Tanzania na timu ya taifa ya Ethiopia iliyomalizika kwa matokeo ya 0-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kwa kuzingatia kwamba Yanga itakuwa ugenini, huku ikifahamika kwamba wachezaji wake 14 walikuwa katika majukumu ya kitaifa hivyo watakuwa na uchovu wa safari dhidi ya timu inayomiliki sana mpira, ni haki kusema kazini kwa Wananchi leo kuna kazi.

REKODI
Yanga ina mziki mzito msimu huu, lakini inafahamu haijawahi kushinda katika ardhi ya Ethiopia na mara ya mwisho Yanga kucheza nchini humo ilikuwa Aprili 18, 2018 ilipolala bao 1-0 mbele ya Welayta Dicha lakini ikafuzu makundi ya Kombe la Shirikisho kwa ushindi wa jumla wa 2-1, kwani ilishinda nyumbani 2-0.
Hata hivyo, Yanga inafahamu inakutana na timu mpya isiyo na rekodi kubwa kulinganisha na wao wakishiriki kwa mara ya kwanza mashindano ya Ligi ya Mabingwa baada ya msimu uliopita kutwaa taji la Ligi Kuu ikiwa pia ni mara ya kwanza ya kwanza tangu klabu hiyo ilipoasisiwa mwaka 1982.
CBE ilitwaa taji hilo ikiwa imejijenga upya mwaka 2021 ikitoka kushuka daraja 2017 inataka kuweka rekodi mpya kujaribu kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu huu, baada ya awali kuing'oa SC Villa ya Uganda kwa jumla ya mabao 3-2, ikianza kushinda ushindi wa mabao 2-1 ugenini na sare ya 1-1 nyumbani.
Kwa upande wa Yanga imetinga hatua hii kibabe ikitoka kuirarua bila huruma Vital'O ya Burundi kwa jumla ya mabao 10-0 na akili ilivyo kwa sasa ni kufika makundi ili kuandika historia ya kutinga msimu wa pili mfululizo, kwani msimu uliopita ilitinga baada ya miaka 25 kupita na kupenya zaidi hadi robo fainali.
CBE haitofautiani sana na falsafa ya Yanga, kwani zote zinacheza soka la kushambulia zaidi, hivyo kufanya mchezo huo wa kesho kuwa aina yake na kushindwa kutabirika mapema, licha ya uzoefu kuibeba Yanga.
Waethiopia hao ina wachezaji watatu wa kigeni katika kikosi wakiwamo Waghana wawili, beki Caleb Amankwah na kiungo Umar Bashiru, huku Simon Oketch akitokea Uganda.

WAAMUZI WOTE SENEGAL
Mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Abebe Bikila, jijini Addis unaochukua mashabiki 25,000 walioketi, utaamuliwa na mwamuzi wa kati, Issa SY kutoka Senegal aliyekuwa hapa nchini wikiendi iliyopita katika mchezo wa Tanzania dhidi ya Ethiopia wa kuwania kucheza Fainali za Mataifa Afrika (Afcon) 2025.
SY amewahi kuamua mechi ya Yanga iliposhinda ugenini dhidi ya Club Africain kwa bao 1-0 kisha kufuzu kibabe hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Novemba 9, 2022 pia aliwahi kuwa mezani Oktoba 20, 2023 wakati Simba ikilazimishwa sare ya 2-2 dhidi ya Al Ahly ya Misri katika African Football League (AFL).
Waamuzi wengine wa mchezo huo wa kesho dhidi ya CBE SA, ni Djibril Camara atakayekuwa mwamuzi wa kwanza msaidizi, Nouha Bangoura atakayekuwa msaidizi wa pili, huku Douda Gueye atakuwa mezani na wote pia wanatokea Senegal, wakati Kamishna wa mchezo ni Michel Gasingwa kutoka Rwanda huku mtathimini wa waamuzi ni Peter Edibe kutoka Nigeria.

MVUA INAPIGA
Yanga ilipotua Ethiopia imekutana na mvua nyingi za vipindi lakini haikuwa habari mpya kwao kwani walishapata taarifa mapema kutoka kwa watu wao waliotangulia kuwa wajiandae na hali hiyo ya hewa.
Kesho Jumamosi hali ya hewa nchini humo inaonyesha itakuwa nyuzi joto 20 ikishuka kutoka 21 ya leo ambapo kutakuwa na mvua za hapa na pale, mawingu na radi kutokana na nchi hiyo ipo kwenye majira ya mkvua nyingi.
HERSI ANATUA NA NENO ZITO
Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said hakuongozana na timu hiyo kama ilivyozoeleka, lakini kesho atawasili nchini humo akitokea Ivory Coast alipohudhuria Mkutano mmoja mkubwa wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) akiwa mjumbe wa mkutano huo kwa kofia ya Rais wa Umoja wa klabu za Afrika.
Hersi hatatua hivi hivi anatarajiwa kushuka na neno zito la ahadi kutoka kwa mfadhili wao Gharib Said Mohammed 'GSM' itakayowafanya mastaa wa timu hiyo kufanya kweli kwenye mchezo huo.

GAMONDI ALIAMSHA
Jana wakati Yanga ikitaka kuanza ratiba ya mazoezi ya kwanza kocha Miguel Gamondi akaliamsha akiwataka wachezaji wa kikosi hicho kuacha kufikiria malengo ya mbali na kwanza waaanze kuiwinda nafasi ya kutinga makundi kuanzia mechi hiyo.
"Sikilizeni nafahamu kila mmoja wenu hapa anawaza kwamba timu yetu itafika mbali kwenye mashindano haya ya Afrika, nataka kuwaambia kitu acheni mawazo hayo kila mmoja arudishe akili yake kwenye mechi hizi mbili zijazo tushinde hapa na nyumbani kisha tuingia makundi huko tutajipanga zaidi kila kitu kinakwenda kwa hesabu," amesema Gamondi.
Akizungumzia mchezo huo, Gamondi amesema malengo yao ni kuhakikisha wanashinda mechi hiyo ingawa hawakupata muda wa kutosha kujiandaa kutokana na ratiba ngumu ya wachezaji wake wengi wa kikosi cha kwanza kukosekana.
"Jambo la kushukuru ni kwamba wachezaji wengi wamerejea wakiwa sawa kiafya lakini hatukupata muda wa kutosha kujiandaa kwa pamoja kwa ajili ya mchezo huu kama ambavyo nilikuwa nasema awali, tuna maandalizi yetu kama timu lakini kuna maandalizi maalum kwa ajili ya mchezo husika hili ndio ninalomaanisha," amesema Gamondi na kuongeza;
"Kuhusu mchezo ni wazi itakuwa mechi ngumu tunacheza na timu nzuri ambayo ina wachezaji vijana na wanaocheza soka la kuvutia, kama watakuja na kucheza mpira itakuwa mechi ngumu na nzuri, tuna timu imara yenye wachezaji wazoefu tunataka kushinda hapa ili kurahisisha mechi ya marudiano."
Kwa upande wa kocha wa CBE SA, Sisay Kumbe ameliambia Mwanaspoti wanakwenda kukutana na timu kubwa yenye wachezaji wazoefu ambapo hata kama rekodi yao ni kubwa wanataka kujaribu kushinda nyumbani kisha kwenda kujipanga na mchezo wa marudiano.
"Huwezi kuilinganisha Yanga na CBE, hii timu yetu ni mpya, tunakwenda kukutana na Yanga ambao wana rekodi kubwa kwenye mashindano haya, wachezaji wao ni wazoefu zaidi, tumejiandaa kuhakikisha tunashinda hapa nyumbani," amesema Kumbe.