Yanga yaongeza deni soka Arusha

Arusha. Ukiachana na ushindi wa mabao 3-1 walioipata Yanga dhidi ya Dodoma Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu, juzi, lakini burudani waliyotoa timu zote imekoleza deni la soka Arusha.
Kabla ya Yanga, Coastal Union ilicheza mchezo wao kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, ambao mashabiki wa soka mkoani hapa waliojitokeza walipaza sauti kwa uongozi wa soka wahakikishe Arusha inakuwa na timu ya Ligi Kuu.
Arusha, ambayo haina timu ya ligi kuu kwa misimu mitano sasa tangu JKT Oljoro ishushwe na kuuzwa kabisa, macho na masikio ya wadau wa soka mkoani hapa yamewekeza matumaini yao kwa AFC, ambayo inasota Daraja la Kwanza miaka mitata sasa.
“Ifikie wakati Arusha tuamue kwa kauli moja kushirikiana tuwe na timu ya Ligi Kuu, sio hizi za kupewa ambazo ratiba zake hazileti maandalizi, hivyo viongozi wa soka Arusha na sisi kwa pamoja tujitafakari nini cha kufanya maana wengine mpira ndiyo ulevi wetu” alisema Lagumbo Gumbo.
Kwa upande wake, wamiliki wa Uwanja wa SheikhAmri Abeid, kupitia katibu mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Gerald Munisi alisema wao wanajitahidi kadri wawezavyo kuhakikisha wanazidi kuboresha uwanja huo.