Yanga yaifuata Bayern Munich

Wachezaji wa Yanga wakishangilia ushindi
Muktasari:
Yanga imetwaa ubingwa ikiwa na ukuta mzito ulioruhusu mabao 14 ikiwa ni machache kuliko timu zote zilizoshiriki Ligi Kuu Bara msimu huu.
UKIANGALIA rekodi za Ligi Kuu kubwa Duniani msimu huu utaanza kuwaona Bayern Munich ambao waliiaibisha Barcelona kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki hii halafu utaiona Man United ya England ukirudi Afrika Mashariki na Bongo, utaikuta Yanga.
Ndizo timu tatu zilizotwaa ubingwa mapema msimu huu zikiwa na mechi mkononi. Yanga imekuwa ya tatu kutwaa taji ukizichambua ligi 10 kubwa Duniani walitawazwa mabingwa wakiwa na pointi 56 na kusaliwa na mechi mbili dhidi ya Coastal Union na Simba.
Timu hiyo ilitoka sare ya bao 1-1 na Coastal, Jumatano iliyopita na kufikisha pointi 57 imeungana na timu kubwa duniani kama Bayern Munich ya Ujerumani iliyokuwa ya kwanza kutwaa ubingwa ikiwa na mechi sita mkononi. Ya pili ni Man United ya England iliyotwaa ubingwa ikiwa imebakiwa na mechi nne mkononi.
Timu nyingine zinazoweza kuifuata Yanga kutwaa ubingwa mapema ni Barcelona yenye pointi 85 ikiwazidi wapinzani wao Real Madrid kwa pointi 11 wakiwa na mechi tano mkononi na muda wowote watatangaza ubingwa wakati Juventus ya Italia nayo ikiwa na uhakika wa kutwaa ubingwa huku wakibakiwa na mechi mkononi lakini wanatakiwa waombee wapinzani wao Napoli wapoteze japo mechi moja tu.
Juventus ina pointi 80, Napoli ina pointi 69 wakati Milan ni ya tatu ikiwa na pointi 62 na zote zimebakisha mechi nne kabla ya msimu wa ligi kumalizika.
Nchini Uholanzi, Ajax itakuwa na uhakika wa kutwaa taji kama itashinda mechi zake mbili zilizobaki au iombee wapinzani wake wapoteze mchezo mmoja tu unaofuata ili wawe mabingwa, wana pointi 70 wanafuatiwa kwa karibu na PSV yenye 66 na Feyenoord 66 pia.
Kwenye ligi 1 ya Ufaransa, PSG wana nafasi kubwa ya kuwa mabingwa, wana pointi 73 wakifuatiwa na Olympique Marseile wenye 64 na Olympique Lyonnais inafuatia kwa kuwa na pointi 60 huku zote zikibakiwa na michezo minne.
Nchini Scotland, Celtic inashika usukani wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 72 ikifuatiwa na Motherwell yenye 60 wakati Inverness CT ni ya tatu ikiwa na pointi 51. Zote zimebakiwa na michezo minne.
Kwenye Ligi Kuu ya Russia, CSKA Moscow inaongoza ikiwa na pointi 57 lakini bado ina kibarua cha kuhakikisha inatwaa ubingwa, wapinzani wake, Zenit wanawafukuzia kwa karibu wakiwa na pointi 54 na Anzi anayoichezea staa wa Cameroon, Samuel Eto’o ikiwa ya tatu kwa kuwa na pointi 47 na zote zikibakiza michezo minne kabla ya ligi kumalizika.
Nchini Brazil Fluminense inaongoza ligi ikiwa na pointi 41, wamecheza michezo 21 wakifuatiwa na Corinthians yenye pointi 38 na Botafogo ya tatu ikiwa na pointi 37 ingawa bado mechi nyingi zimebaki kabla ya ligi hiyo kumalizika.
Argentina, Velez Sarsfield wanaongoza, wana pointi 41 wamecheza michezo 19 wakifuatiwa na Newell’s Old Boys wenye pointi 36 na Belgrano ya tatu ikiwa na pointi 36 pia na bado wana michezo mingi kabla ya ligi kumalizika.
Yanga imetwaa ubingwa ikiwa na ukuta mzito ulioruhusu mabao 14 ikiwa ni machache kuliko timu zote zilizoshiriki Ligi Kuu Bara msimu huu.
Kipa alikuwa Ally Mustapha ‘Barthez’, mabeki wa kati Kelvin Yondani ‘Vidic’, Nadir Haroub ‘Canavaro’, mabeki wa pembeni Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Juma Abdul na David Luhende.
Mabingwa hao wamepachika wavuni mabao 44 kuliko timu yoyote kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu ingawa bado kocha mkuu Ernest Brandts amedai hajaridhishwa na kiwango cha washambuliaji hao. Timu hiyo ina mabao 10 zaidi ya wapinzani wao Simba.