Prime
Mpanzu, wenzake wana wiki mbili tu

Muktasari:
- Hatua ya mastaa hao kupewa likizo fupi imeelezwa kutokana na mipango aliyonayo Kocha Fadlu Davids kutaka kuanza kunoa makali mapema ili msimu ujao warejee kivingine na kurejesha heshima ya kubeba mataji na pia kutamba kimataifa.
SIKU chache tangu washindwe kuhimili kishindo cha Yanga na kukubali kichapo cha mabao 2-0 wakifunga msimu wa 2024-2025 bila taji, mastaa wa Simba akiwamo Elli Mpanzu na Jean Charles Ahoua wamepewa wiki mbili za kupumzika kabla ya kurejea kujiandaa na msimu ujao.
Hatua ya mastaa hao kupewa likizo fupi imeelezwa kutokana na mipango aliyonayo Kocha Fadlu Davids kutaka kuanza kunoa makali mapema ili msimu ujao warejee kivingine na kurejesha heshima ya kubeba mataji na pia kutamba kimataifa.
Simba ilimaliza msimu kwa kufumuliwa na Yanga katika Dabi ya Kariakoo iliyoahirishwa mara mbili, Machi 8 na Juni 15 na kushika nafasi ya pili ikikusanya pointi 78 baada ya mechi 30, huku ikilikosa taji la Ligi Kuu baada ya awali kukosa Ngao ya Jamii na Kombe la Shirikisho (FA).
Inaelezwa kitendo cha kumaliza kinyonge kumemfanya Fadlu kuwabana mastaa wa timu hiyo kwa kuwapa muda mfupi wa kupumzika kabla ya kurejea mapema kuanza mipango mipya ikiwamo kuwahi kambini kusikilizia msimu mpya.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zimelidokeza Mwanaspoti kuwa, kikosi hicho kitakuwa na mapumziko ya wiki mbili.
“Mastaa wote watapumzika wiki mbili,lakini baada ya hapo watakuwa na muda wa mazoezi binafsi kabla ya kwenda kwenye maandalizi ya msimu ujao. Bado ratiba haijakaa sawa na haijajulikana kuwa ni wapi watakwenda kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao,” kilisema chanzo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa kikosi hicho, Patrick Rweymamu alisema kuwa mastaa wa timu hiyo wamepewa muda wa siku kadhaa kupumzisha miili.
“Bado ratiba haijatoka ya mapumziko hivyo tunamsubiri kocha atuambie kinachofuata ila kwa sasa tunamapumziko mafupi ya kutuliza akili,” alisema.
Wekundu hao msimu huu hawajaambulia chochote kwani wamekosa makombe yote wakianza na Ngao ya Jamii, wakifuatiwa na Kombe la Shirikisho, Ligi Kuu Bara na FA
Timu hiyo imemaliza msimu ikiwa na rekodi ya kufundishwa na kocha - Msauzi ambaye ni Fadlu Davids na benchi lake la ufundi, huku katika msimamo wa ligi ikiwa imeshika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 78, ikicheza mechi 30, imeshinda 25, sare tatu na kupoteza mbili ikifunga mabao 56.