Prime
Fainali ya FA Yanga v Singida BS vita ipo hapa

Muktasari:
- Safari hii itakuwa fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) itakayofanyika Jumapili ya Juni 29, 2025 kuanzia saa 2:15 usiku. Mara ya mwisho timu hizo zilikutana uwanjani hapo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara duru la kwanza uliochezwa Oktoba 30, 2024, Yanga ikashinda bao 1-0 lililofungwa na Pacome Zouzoua dakika ya 68.
ZANZIBAR: IMEPITA takribani miezi minane sawa na siku 243 tunarudi tena New Amaan Complex, Zanzibar kushuhudia Singida Black Stars ikicheza dhidi ya Yanga.
Safari hii itakuwa fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) itakayofanyika Jumapili ya Juni 29, 2025 kuanzia saa 2:15 usiku. Mara ya mwisho timu hizo zilikutana uwanjani hapo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara duru la kwanza uliochezwa Oktoba 30, 2024, Yanga ikashinda bao 1-0 lililofungwa na Pacome Zouzoua dakika ya 68.
Katika mchezo huu uliobeba hisia za mashabiki wa soka kutoka kisiwani hapa na maeneo yote ya Tanzania na nje ya mipaka, tutashuhudia ushindani mkubwa ikizingatiwa ndiyo mchezo wa mwisho msimu huu 2024-2025 kws timu hizi.
ILIPO MECHI
Vita kubwa katika fainali hii itakuwa eneo la kati kwenye kiungo, sehemu ambayo wachezaji wanatengeneza mikakati ya kupandisha timu kwenda kufunga mabao ikionekana pande zote zinajiweza. Silaha ya Yanga eneo hilo ipo kwa Khalid Aucho, Duke Abuya na Mudathir Yahya, wachezaji ambao Kocha Miloud Hamdi amekuwa na tabia ya kuwaanzisha pamoja pale katikati.
Aucho na Duke, kazi yao kubwa ni kusaidia kuzuia mashambulizi ya wapinzani, huku Mudathir akiongeza nguvu katika kushambulia hali inayomfanya kufunga mara kwa mara. Wakati mwingine Mudathir anarudi chini, Duke anapanda juu, ubora wa viungo hawa katika kuzuia na kushambulia unaifanya Yanga kuwa imara pale katikati. Pembeni, Yanga ina Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua, kisha pale mbele kwenye ushambuliaji Prince Dube na Clement Mzize anaweza kuanza mmoja kama ilivyokuwa mechi iliyopita dhidi ya Simba, au kucheza pamoja kama walivyofanya nusu fainali ya FA walipoichapa JKT Tanzania.
Hata hivyo, anapoanza Dube na Mzize, kocha hulazimika kumpumzisha kiungo mmoja kati ya Abuya na Mudathir.
Singida Black Stars inayofundishwa na David Ouma, inaye Emmanuel Keyekeh, Arthur Bada na Mohamed Damaro wanaoimarisha eneo la kiungo, wakati mwingine anacheza Morice Chukwu au Kelvin Nashon kwenye nafasi mojawapo.
Eneo la ushambuliaji, kuna mchezaji tegemeo, Jonathan Sowah, mwamba aliyeingia dirisha dogo la usajili msimu huu akamaliza na mabao 13 kwenye Ligi Kuu Bara, matatu nyuma ya kinara Jean Charles Ahoua wa Simba. Makali ya Sowah aliyefunga bao pekee walipofungwa 2-1 mara ya mwisho kwenye ligi, yatawashughulisha vilivyo walinzi wa kati wa Yanga, nahodha msaidizi Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’.
Lakini pia hata walinzi wa Singida Black Stars, Andé Koffi Cirille, Frank Asinki, Anthony Tra Bi Tra n Ibrahim Imoro watakuwa na kazi ya kumlinda kipa wao, Amas Obasogie asifikiwe na balaa na Mzize, Dube waliofunga kila mmoja Yanga iliposhida 2-1 mara ya mwisho dhidi ya Singida Black Stars, pia Pacome aliyewaadhibu walipokutana duru la kwanza.
TUMEFIKAJE HAPA?
Imekuwa safari ndefu kuanzia hatua ya 64 bora hadi sasa fainali zimebaki timu mbili zinazowania ubingwa wa michuano hii ya pili kwa ukubwa Tanzania ngazi ya klabu baada ya Ligi Kuu Bara. Yanga kwa kufika fainali ikienda kutetea taji, imegawa dozi tofautitofauti dhidi ya wapinzani iliokutana nao kuanzia hatua ya 64 bora hadi nusu fainali ikicheza mechi tano. Ilianza kwa kuichapa Copco mabao 5-0, kisha Coastal Union (3-1), Songea United (2-0), Stand United (8-1) na JKT Tanzania (2-0). Katika mechi hizo tano, Yanga imefunga mabao 20, huku nyavu zake zikitikiswa mara mbili pekee, ikiambulia clean sheet tatu.
SINGIDA WAGENI TUPU
Ukiachana na bao la kujifunga kupitia beki wa KMC, Abdallah Said ‘Lanso’ katika mchezo wa hatua ya 16 bora lililoipa ushindi Singida Black Stars 1-0 na kufuzu robo fainali kutokana na zawadi hiyo ya mchezaji mzawa, mengine yaliyobaki kwa timu hiyo yamefunga na wachezaji wa kigeni.
Singida Black Stars iliyovuna mabao 12 katika mechi tano za michuano hii kuanzja hatua ya 64 bora hadi nusu fainali, mabao 11 wafungaji ni wageni wote. Wafungaji wa mabao hayo ni Emmanuel Keyekeh (3), Marouf Tchakei (2), Jonathan Sowah (2), Josephat Bada (1), Elvis Rupia (1), Hernest Malonga (1) na Victorien Adebayor (1).
Wakati Singida Black Stars ikiwa hivyo, kwa upande wa Yanga mabao yake 20 yamegawanyika kwa wazawa wakifunga matano na wageni wamepachika mabao 15.
Wafungaji wazawa ni Mudathir Yahya (2), Sheikhan Ibrahim (1), Clement Mzize (1) na Nickson Kibabage (1). Wageni waliofunga ni Stephane Aziz Ki (4), Maxi Nzengeli (3), Prince Dube (2), Duke Abuya (2), Clatous Chama (2), Jonathan Ikangalombo (1) na Kennedy Musonda (1).
MABAO YAPO HAPA
Katika fainali hii, tunaweza kushuhudia mabao yakipatikana zaidi kipindi cha pili kutokana na rekodi zilivyo kwa timu zinazokwenda kupambana.
Ukiangalia Yanga katika mabao yake 20 iliyofunga kwenye michuano hii, imejitahidi kuyagawa, kipindi cha kwanza imefunga 10 na cha pili idadi kama hiyo.
Singida Black Stars imekuwa tofauti kwani mabao manne imefunga kipindi cha kwanza na manane kipindi cha pili.
Kwa ujumla, Yanga na Singida Black Stars zimechangia mabao 32, ambapo 14 yamefungwa kipindi cha kwanza na 18 kipindi cha pili.
NI HESHIMA, REKODI
Tangu Julai 25, 2021, Yanga ilipofungwa 1-0 na Simba katika fainali ya michuano hii, imecheza mechi 21 mfululizo za Kombe la FA bila kupoteza. Hii ni fainali ya tano kwa Yanga kucheza mfululizo, ambapo katika nne zilizopita imeshinda tatu na kupoteza moja. Pia Yanga ndiyo timu iliyocheza fainali nyingi za michuano hii tangu 2015-2016 ambazo ni tano, hii inakuwa ya sita. Kitu pekee ambacho Yanga inakwenda kukifanya mbele ya Singida Black Stars ni kuweka heshima na rekodi ya kutetea taji ililobeba misimu mitatu mfululizo. Yanga ndiyo bingwa mara nyingi wa michuano hii tangu iliporejea msimu wa 2015-2016 ikichukua mara nne (2015-2016, 2021-2022, 2022-2023 na 2023-2024). Inasaka la tano.
Inafuatia Simba iliyobeba mara tatu (2016-2017, 2019-2020 na 2020-2021), kisha Mtibwa Sugar (2017-2018) na Azam (2018-2019). Kwa upande wa Singida Black Stars, inasaka rekodi ya kuchukua taji la kwanza tangu kuanzishwa kwa timu hiyo, huku pia ikihitaji kulipa kisasi mbele ya Yanga. Rekodi zinaonesha msimu huu timu hizo zimekutana mara mbili katika mechi za mashindano zote ikiwa kwenye Ligi Kuu Bara ambapo Yanga imeibuka kidedea.
Mechi ya kwanza ilishinda 1-0 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kwa bao la Pacome Zouzoua, kisha ikashinda 2-0 pale KMC Complex, Dar.
Singida Black Stars si tu kusaka ushindi mbele ya Yanga, bali inatafuta kufunga bao la kwanza dhidi ya wapinzani wao hao kwani mechi mbili zilizopita imetoka patupu.
SASA ITAKUWAJE?
Katika fainali nne za FA ilizocheza Yanga, zimekuwa za kushangaza kidogo kutokana na aina ya matokeo yake. Imeshuhudiwa fainali mbili zikimalizika ndani ya dakika tisini mshindi akipatikana kwa ushindi wa bao 1-0. Hiyo ilikuwa msimu wa 2020-2021 ilipopoteza mbele ya Simba kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, kisha 2022-2023 ilipoichapa Azam 1-0 pale Mkwakwani, Tanga.
Fainali zingine mbili zilimalizika kwa mikwaju ya penalti baada ya kwenda hadi dakika 120 matokeo yakiwa sare. Safari hii itakuwaje?