Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga Waarabu, Simba washindwe wenyewe

Muktasari:

  • Droo ya upangaji wa hatua ya makundi kwa mashindano hayo yote mawili itachezeshwa Oktoba 7 huko Cairo, Misri.

BAADA ya kufuzu kibabe hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika, Yanga na Simba kuna uwezekano mkubwa zikakutana na wapinzani wenye uzito tofauti baada ya droo ambayo itapangwa mapema mwezi ujao.

Droo ya upangaji wa hatua ya makundi kwa mashindano hayo yote mawili itachezeshwa Oktoba 7 huko Cairo, Misri.

Yanga itakuwa katika chungu cha pili katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambacho pia kina timu za Raja Casablanca, Pyramids na CR Belouizdad.

 Chungu cha kwanza kina Al Ahly, TP Mazembe, Esperance na Mamelodi Sundowns huku chungu cha tatu kikiwa na timu za Al Hilal, Orlando Pirates, Sagrada Esperanca na AS FAR wakati huo katika chungu cha nne kutakuwa na Maniema, Stade d’Abidjan, MC Alger na Djoliba.

Kwa kuwekwa chungu cha pili, Yanga kuna uwezekano wa kupangwa katika kundi moja na timu tatu kutoka katika nchi zinazozungumza lugha ya Kiarabu ambazo kwa muda mrefu zimetawala soka la Afrika.

Kutakuwa na vyungu vinne katika upangaji wa makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo timu moja katika kila chungu zitaunda kundi moja la mashindano hayo na timu zilizopo katika chungu kimoja haziwezi kukutana.

Wakati Yanga ikiwa na uwezekano wa kukutana na Waarabu watatu kwenye kundi lake, watani wao Simba wanaonekana kuwa katika nafasi nzuri ya kuumana na timu zisizo tishio sana au zisizo na uzoefu kwenye Kombe la Shirikisho.

Katika Kombe la Shirikisho Afrika, kutakuwa na vyungu vitatu ambapo katika uchezeshaji wa droo, timu moja kutoka katika chungu cha kwanza itaungana na nyingine moja ya chungu cha pili na mbili kutoka chungu cha tatu kuunda kundi moja ambapo timu zilizopo katika chungu cha kwanza na cha pili haziwezi kupangwa katika kundi moja.

Kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Simba itakuwa katika chungu cha kwanza na timu za Zamalek, USM Alger na RS Berkane, chungu cha pili kikiwa na timu za Asec Mimosas, Stade Malien, Al Masry na CS Sfaxien na chungu cha tatu kina timu za Enyimba, ASC Jaraaf, Bravos Maquis, Lunda Sol, Orapa, Black Bulls na Stellenbosch.

Ifahamike kuwa hii ni mara ya kwanza katika historia ya mashindano ya klabu Afrika kwa Yanga kuwa katika chungu cha pili kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kama ilivyo kwa Simba kuwa katika chungu cha kwanza kwenye Kombe la Shirikisho Afrika .

Kwa kuwekwa katika chungu cha kwanza, Simba itaanzia mechi za hatua ya makundi nyumbani na itamalizia nyumbani kama ilivyo kwa Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Heshima kwa wapinzani

Mashabiki wa Yanga na Simba kwa sasa wanatabasamu baada ya timu hizo kutinga hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika ambayo mechi zake zitaanza kuchezwa mwezi ujao, lakini bila shaka hali ni tofauti kwa makocha wao.

Vichwani mwa makocha Miguel Gamondi wa Yanga na Fadlu Davids wa Simba kwa sasa akili zao zinawaza ni kwa namna gani wataandaa timu zao ili ziweze kutamba katika hatua hiyo ya makundi na kutinga robo fainali au hatua za juu zaidi ya hiyo.

Na hilo linatokana na uwepo wa timu nyingi zenye uzoefu na historia ya mwendelezo wa kufanya vizuri katika mashindano ya klabu Afrika.

Uthibitisho wa hilo ni uwepo wa timu chache tu ambazo hazijawahi kucheza hatua ya makundi kati ya 32 zilizoingia kwenye hatua hiyo msimu huu, kumi na sita zikiwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na 16 nyingine katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Ni timu tisa tu ambazo zinashiriki kwa mara ya kwanza katika hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika kati ya 32 huku nyingine 23 zikiwa tayari zimeshafanya hivyo na baadhi hadi ziliwahi kutwaa ubingwa.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, timu tatu zinashiriki kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ambazo ni Sagrada Esperanca, Maniema na Stade d’Abidjan.

Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika timu sita ambazo zinashiriki kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ni ASC Jaraaf, Bravos Maquis, Lunda Sol, Orapa, Black Bulls na Stellenbosch.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, timu 13 zimewahi kucheza hatua ya makundi au za juu zaidi ambazo ni Yanga, Al Ahly, Esperance, Mamelodi, TP Mazembe, Pyramids FC, Al Hilal, Orlando Pirates, AS FAR, MC Alger, Raja Casablanca, CR Belouizdad na Djoliba.

Kombe la Shirikisho Afrika litakuwa na timu 10 ambazo ziliwashawahi kuingia hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika au kwenda hatua za juu zaidi ambazo ni Simba, Zamalek, RS Berkane, USM Alger, Asec Mimosas, Stade Malien, Asec Mimosas, Enyimba, Al Masry, CS Constantine na CS Sfaxien.


SHUGHULI IKO MLANGONI

Raundi mbili za mwanzo za hatua ya makundi katika mashindano yote zitaanza kuchezwa mwezi ujao na raundi ya tatu na ya nne zitachezwa Novemba huku mbili za mwisho zikichezwa Desemba.

Yanga katika mechi ya kwanza itacheza na timu kutoka chungu cha tatu, mechi ya pili na timu kutoka chungu cha nne huku mechi ya tatu na ya nne ikicheza dhidi ya timu ya chungu cha kwanza.

Mechi ya tano itacheza na timu ya chungu cha tatu na itamaliza dhidi ya timu ya chungu cha nne.

Simba itaanza na timu ya nne kwenye kundi kisha itacheza na timu ya tatu katika kundi na mechi mbili zinazofuata itakutana na timu ya chungu cha pili.

Mechi ya tano itakabiliana na timu ya nne na ya mwisho ni dhidi ya timu ya tatu.