Yanga kwa magoli! Wamepoteza mbaya

Muktasari:
Wachezaji hao wamezifunika karibu klabu zote za Ligi Kuu Bara zikiwamo Simba, Azam na Mtibwa Sugar waliopo Nne Bora.
YANGA leo Jumamosi itakuwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kucheza mchezo wa marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius, lakini katika kikosi chake kina watu watano funika bovu.
Wachezaji hao wamezifunika karibu klabu zote za Ligi Kuu Bara zikiwamo Simba, Azam na Mtibwa Sugar waliopo Nne Bora.
Usiumize kichwa, ipo hivi. Hebu angalia msimamo wa Ligi Kuu Bara, utaiona Yanga ipo kileleni ikiwa na pointi zake 46 kama ilivyo Azam, lakini ina idadi kubwa ya mabao ya kufunga (44) ni mengi kwelikweli kuliko timu zote shiriki za ligi hiyo.
Achana na hiyo, rejea kwenye orodha ya wafungaji wa ligi hiyo utayaona majina ya Amissi Tambwe akishika nafasi ya pili akiwa na mabao 15, nyuma ya Hamis Kiiza wa Simba mwenye mabao 16.
Ukisogea chini kidogo utaliona jina la Donald Ngoma, pia wa Yanga mwenye mabao 11 akibanana na Jeremiah Juma wa Prisons. Mfungaji Bora wa msimu uliopita, Simon Msuva anayo mabao sita, huku kiungo Thabani Kamusoko akiwa na mabao matano na Malimi Busungu naye akiwa na mabao mawili.
Hapo hajawekwa Paul Nonga mwenye mabao matano kwani alihama nayo kutoka Mwadui.
Sasa ebu jumlisha tu mabao ya Tambwe 15 na yale 11 ya Ngoma utapata mabao mangapi? Jumla ni mabao 26 ambayo ni zaidi ya nusu ya mabao yote ya Yanga. Lakini idadi hiyo ni kubwa kwani timu nyingine 13 ukiondoa Azam na Simba zimeshindwa kuyafikia katika mechi zao za raundi 20 zilizochezwa mpaka sasa katika ligi hiyo.
Mtibwa Sugar na Mwadui zenyewe zina mabao 21, Mbeya City (20), Prisons (19) sawa na Ndanda, Stand United, JKT Ruvu na Toto Africans, Mgambo ina mabao 16, Copastal ina mabao 13, huku Majimaji ina mabao 12 kisha Kagera yenye 11 na African Sports ina buruza mkia ikiwa na mabao saba tu.
Ukiyajumlisha mabao ya Tambwe na Ngoma na yale 13 ya Msuva, Kamusoko na Busungu maana yake utapata jumla ya mabao 39 ambayo ni mengi kuliko iliyonayo Azam (34) na Simba (35). Sasa kwa nini wakali hao watano wasiwe funika bovu? Takwimu hizo zinaifanya Yanga kuwa timu pekee yenye safu kali ya ushambuliaji nchini kwa msimu huu na pengine kile kiapo cha Kocha wake, Hans Pluijm kwamba anataka kufikisha mabao 70 kinaweza kutimia. Pluijm alisema angependa msimu huu kutwaa ubingwa na idadi kubwa ya mabao ili kuvunja rekodi zote za nyuma. Kama vijana wake watakaza mwendo kuna uwezekano wa kuyapata kwani Yanga ina mechi 11 mkononi kwa sasa.
Safu inayoifuata Yanga kwa idadi kubwa ya mabao ni Simba ambayo washambuliaji wake watatu; Kiiza, Ibrahim Ajib na Danny Lyanga, wamefunga jumla ya mabao 24, huku Azam ikishika nafasi ya tatu ikiwa na mabao 22 ikijumuisha mabao ya Kipre Tchetche (9), John Bocco (7), Didier Kavumbagu (4) na mawili ya Farid Mussa (2).
Hata hivyo Azam pia ina mabao mengine yaliyotupiwa na beki Shomari Kapombe amefunga mabao saba na kiungo Frank Domayo ameifungia mawili.
Kwa sasa Ligi Kuu imesimama hadi Jumanne kwa kuchezwa mchezo wa kiporo cha Yanga na Mtibwa kitakachochezwa Machi Mosi kabla ya Jumamosi ijayo kuendelea kwa michezo mingine ukiwamo wa Yanga na Azam utakaomaliza ubishi kati yao.
Timu hizo mbili ndizo zinazochuana kwenye mbio za ubingwa na kwa misimu mitatu mfululizo zimekuwa zikokezana nafasi mbili za juu wakiiengua Simba.