Mtibwa yaiwinda saini ya beki Coastal Union

Muktasari:
- Zambo, ambaye pia ni nahodha wa kikosi hicho baada ya kuondoka kwa Jackson Shiga aliyejiunga na Fountain Gate, mkataba alionao na Coastal Union unafikia tamati mwisho wa msimu huu, huku kukiwa pia hakuna mazungumzo yanayoendelea na timu hiyo.
BAADA ya Mtibwa Sugar kurejea tena Ligi Kuu baada ya kushuka msimu uliopita, mabosi wa timu hiyo wako katika mchakato wa kuboresha kikosi hicho, ambapo tayari wanampigia hesabu kali beki wa kushoto wa Coastal Union, Miraji Abdallah ‘Zambo’.
Zambo, ambaye pia ni nahodha wa kikosi hicho baada ya kuondoka kwa Jackson Shiga aliyejiunga na Fountain Gate, mkataba alionao na Coastal Union unafikia tamati mwisho wa msimu huu, huku kukiwa pia hakuna mazungumzo yanayoendelea na timu hiyo.
Taarifa kutoka Coastal zimeliambia Mwanaspoti nyota huyo, hayupo tayari kuendelea kubakia ndani ya kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao, licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na viongozi ili kumshawishi kuendelea kubaki kikosini.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mtibwa Sugar, Swabri Aboubakar hivi karibuni katika mahojiano yake na Mwanaspoti, alisema baada ya lengo la kuipandisha timu hiyo kufanikiwa, kwa sasa wanaangalia namna nzuri ya kutengeneza pia kikosi cha ushindani.
“Wachezaji tulionao ni wazuri sana na wamepambana hadi kufikia malengo, ila kama unavyojua pia Ligi ya Championship na Ligi Kuu Bara ni tofauti sana, hivyo ni lazima tujipange vizuri kuanzia usajili wetu na mambo mengine,” alisema Swabri.
Mtibwa ambao ni mabingwa wa Championship baada ya kumaliza na pointi 71 na kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka msimu uliopita, wanampigia hesabu nyota huyo ambaye inaelezwa pia hajafanya uamuzi wa sehemu atakayoicheza msimu ujao.