Kaseja, mastaa wang’ang’aniwa Kagera

Muktasari:
- Hatua hiyo imeelezwa ina lengo la kuanza mikakati ya mapema ya kuhakikisha timu hiyo inacheza Ligi ya Championship kisha kurudi Ligi Kuu mapema kama ilivyotokea kwa ‘ndugu’ zao wa Mtibwa Sugar iliyoshuka msimu uliopita na kurejea kwa msimu ujao.
KAGERA Sugar inaendelea kujifua ili kumalizia mechi mbili za mwisho za Ligi Kuu Bara kabla ya kuanza kujiandaa na msimu mpya wa Ligi ya Championship baada ya kushuka daraja, lakini mabosi wa klabu hiyo wameamua kufanya jambo moja la kuwang’ang’ania kocha Juma Kaseja na mastaa kadhaa.
Hatua hiyo imeelezwa ina lengo la kuanza mikakati ya mapema ya kuhakikisha timu hiyo inacheza Ligi ya Championship kisha kurudi Ligi Kuu mapema kama ilivyotokea kwa ‘ndugu’ zao wa Mtibwa Sugar iliyoshuka msimu uliopita na kurejea kwa msimu ujao.
Mkurugenzi Mtendaji wa klabu hiyo, Thabit Kandoro aliliambia Mwanaspoti kuwa, wamepanga kumbakisha kocha Kaseja anayeinoa kwa sasa kumalizia msimu wa Ligi Kuu, sambamba na baadhi ya mastaa bora wa kikosi hicho ili wasipoteze ubora wao wa kuipigania timu kurudi katika ligi hiyo.
Kagera iliyokuwa na msimu mbaya wa Ligi Kuu, imeshuka daraja kabla hata haijamaliza mechi zake ikishika nafasi ya 15 ikiwa na pointi 22 ikiwa sambamba na KenGold iliyoichezea ligi hiyo kwa msimu mmoja baada ya kupanda ikiwa pamoja na Pamba Jiji.
Kandoro alisema wanataka kuwabakisha wachezaji wao bora ili wairudishe katika mashindano ya Ligi Kuu.
Alisema, anafahamu wapo wachezaji waliofanya vizuri, hivyo kama zitakuja ofa nzuri hawatawazuia kuondoka.
“Kagera imejipanga kurudi Ligi Kuu kwa kuwa makosa yetu tuliyoyafanya katika kila idara tumeshayajua, hivyo msimu ujao tunajipanga vizuri zaidi ili tuweze kufanikisha mipango yetu,” alisema Kandoro na kuongeza;
“Jambo zuri hata kocha wetu Kaseja tutabaki naye kwani bado anatufaa sana kutokana na kile ambacho amekifanya katika msimu huu.”
Kaseja aliyekuwa kocha wa makipa amekiongoza kikosi hicho katika mechi tano, ikishinda moja na kupoteza nne na sasa kimesaliwa na mechi mbili za kukamilisha ratiba zote ikicheza ugenini ikianza kuvaana na Namungo siku ya Juni 18, kisha kumalizana na Simba Juni 22 ikiwa ni ya kufungia msimu.