Yanga kama Mamelodi Sundowns tu

Muktasari:

  • Yanga imefuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza tangu muundo wa mashindano hayo ulipobadilika mwaka 2017.

Yanga na Mamelodi Sundowns zimejikuta zimeangukia kwenye mtego mmoja licha ya zote mbili kuwa tayari zimeshajihakikishia kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Mtego ambao unazikabili timu hizo mbili ni ule wa kuhakikisha zinapata ushindi katika mechi zao za mwisho kwenye makundi yao ili ziweze kumaliza zikiwa vinara wa hayo makundi.

Mamelodi Sundowns iliyopo kundi A, ina pointi 10 sawa na vinara wa kundi hilo TP Mazembe na inatakiwa kupata ushindi kwenye mechi ya mwisho baina yao itakayochezwa Afrika Kusini ili imalize ikiwa kinara wa kundi hilo.

Mchezo wa kuamua ni timu ipi kati ya Mamelodi na Mazembe itamaliza ikiwa kinara wa kundi, itachezwa Jumamosi, Machi 02 katika Uwanja wa Loftus Versfeld, Pretoria na Mamelodi itakuwa mwenyeji.

Ikumbukwe TP Mazembe inaongoza kundi hilo licha ya kuwa pointi sawa na Mamelodi Sundowns ikibebwa na kanuni ya kupata matokeo mazuri kwenye mechi baina yao na mechi ya kwanza zilipokutana, Mamelodi ilifungwa bao 1-0.

Kwa upande wa Yanga ili imalize ikiwa kinara wa kundi D, inatakiwa kupata ushindi katika mechi ya mwisho ugenini dhidi ya Al Ahly, jijini Cairo, Misri, Machi Mosi.

Al Ahly inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi tisa na Yanga ina pointi nane.

Timu inayomaliza ikiwa ya kwanza kwenye kundi lake, katika hatua ya robo fainali inakutana dhidi ya timu ambayo imeshika nafasi ya pili.

Mbali na hilo, timu inayoshika nafasi ya kwanza, kwenye hatua ya robo fainali inaanzia ugenini na kumalizia nyumbani.