Yanga, Fei Toto mchuano unaendelea TFF

Muktasari:
- SHAURI la kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Feitoto’ na Yanga bado linaendelea katika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ chini ya Kamati ya Sheria na hadhi za wachezaji wa soka Tanzania.
SHAURI la kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Feitoto’ na Yanga bado linaendelea katika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ chini ya Kamati ya Sheria na hadhi za wachezaji wa soka Tanzania.
Kinachojadiliwa hapo tangu saa 5:00 asubuhi ni shauri la Yanga kumshitaki Feisal kwa kutoonekana kambini na kuwaaga mashabiki wa timu hiyo huku mchezaji mwenyewe akidai tayari amevunja mkataba na Wanajangwani hao na sasa yupo huru.
Katika kesi hiyo, Feisal yupo na Wanasheria wawili ambao pia walisimamia kesi ya Benard Morrison dhidi ya Yanga na kushinda, Makubi Kunju Makubi na Ndurumah Keya Majembe, huku kwa upande wa Yanga wakiwa wanne wakiongozwa na Simon Patrick sambamba na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Andrew Mtine wakati kamati ikiwa na viongozi wengine akiwemo Boniphace Wambura.
Mahojiano ya kwanza baina ya pande zote tatu (Yanga, Feisal na TFF) yalidumu kwa dakika 40, kuanzia saa 5:15 hadi 5:55 na baada ya hapo walitoka nje kupumzika kama dakika tano hivi kisha kurudi tena ndani hadi saa 7:00 walipotoka kwaajili ya kupata chakula na wengine kwenda kuswali, shughuli iliyochukua muda wa saa moja na nusu.
Saa 8:50 mchana waliingia tena ndani ya chumba kile wote kila upande kwa kundi lake na kuanza kujadili kwa kina suala hilo ambapo Mwanaspoti limepenyezewa walikuwa wakijadili hoja baada ya hoja kutoka upande wa Feisal na Yanga.
Hadi saa 11:10 jioni, wote walikuwa bado ndani ya chumba kimoja wakiendelea na majadiliano na Mwanaspoti linaendelea kufuatilia kwa kina ili kuhakikisha linakupa taarifa kamili pale shauri hilo litakapo tamatika au kuahirishwa.