Winga Simba malengo yametimia

WINGA wa Simba, Jimmyson Mwanuke (25) anayecheza kwa mkopo Mtibwa Sugar, amefunguka kwamba malengo ya kwenda Manungu yamelipa kwa kupata nafasi ya kucheza mechi za Ligi Kuu tofauti na alivyokuwa akisugua benchi Msimbazi.
Nyota huyo wa zamani wa Gwambina, alipelekwa kwa mkopo Mtibwa katika dirisha dogo baada ya kukosa namba katika kikosi cha kwanza cha Simba tangu atue misimu miwili iliyopita, lakini akiwa na wababe hao wa zamani wa soka nchini, ametumika kwenye mechi saba kitu kilichomfurahisha.
Mwanuke alisema lengo la kuondoka Simba kwenda Mtibwa ilikuwa ni kulinda na kurejesha makali na kitu hicho ni kama kimefanikiwa hadi sasa, japo timu iliyopo inapambana kuepuka kushuka daraja, ila anafurahi amepata utulivu na nafasi ya kucheza kwa muda mwingi tofauti na alivyo Msimbazi.
"Simba zililetwa ofa nyingi, niliangalia vitu vingi, najua Mtibwa ipo nafasi mbaya kwenye msimamo wa Ligi Kuu hivyo nilihitaji kuipambania na siyo kwenda timu nikaridhika kuona sina kitu cha kufanya," alisema Mwanuke na kuongeza;
"Tangu nijiunge na Mtibwa timu imecheza mechi saba za ligi, nimecheza zote na hilo ndilo lengo langu kupata muda mwingi wa kucheza na tayari nimefunga mabao mawili katika mechi za ASFC. Hapa ingawa huwezi kufananisha na Simba, ila sijaona geni kwani kabla sijawa na Wanamsimbazi nilitokea Gwambina ambako maisha yalikuwa kama haya ninayoishi sasa."
Alizungumzia pia kuhusiana na mkataba wake na klabu ya Simba akisema atakapomaliza kuitumikia Mtibwa ikiwa ni miezi sita aliyokuwa amesalia nayo Msimbazi, atakuwa huru kwani atamalizana nao jumla.