Wasanii kukutana Dar kujadili urasimishaji sanaa

Muktasari:

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Mashirikisho ya Sanaa (Shirikisho la Muziki, Sanaa za Maonesho, Ufundi na Filamu) na wadau wa Sekta ya Sanaa nchini limeandaa Mkutano Mkuu wa Sekta ya Sanaa wenye lengo la kutoa fursa ya kujadiliana kwa pamoja namna bora ya kufikia azma ya urasimishaji wa Sekta ya Sanaa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Katibu Mtendaji wa Basata, Mtiko Mniko amesema lengo kuu la mkutano huo uliobeba kaulimbiu ya ‘Sanaa ni Biashara’ ni kujadili kwa pamoja masuala yahusuyo maendeleo ya sekta ya sanaa nchini.

Mniko amesema malengo ya mkutano huo ni pamoja na kutoa fursa kwa wasanii na wataalamu wa tasnia mbalimbali za sanaa kuwasilisha mawazo na ushauri wa namna bora ya kukuza, kuendesha na kusimamia sekta ya sanaa nchini.

Pia kutoa fursa kwa wadau mbalimbali wa sekta ya Sanaa na kushauri namna bora ya kuendesha shughuli za Sanaa Kibiashara na kuimarisha mahusiano kati ya Serikali, Wasanii na wadau wa Sekta ya Sanaa nchini.

Hata hivyo amesema katika mkutano huo pamoja na mambo mengine, watazindua mfumo mpya wa wasanii wa kujisajili Basata kwa njia ya kielekroniki.

Kwa upande wake Cythncia Enjewele ambaye ni mjumbe wa Shirikisho la Sanaa za Maonesho amewapongoza Basata kwa kuandaa mkutano huo na kuwashauri wasanii kujitokeza kwa wingi  na  fursa hiyo kutoa mawazo yao ni kwa jinsi gani Sanaa itabadilishwa kuwa biashara.