Wanachama Yanga wapewa mchongo

Tuesday June 22 2021
wanachama yanga
By Clezencia Tryphone

BADO siku kama tano tu kabla ya Yanga kuandika historia wakati wanachama wake watakapokutana kwenye Mkutano Mkuu Jumapili wiki hii ili kupitisha mabadiliko yatakayoifanya klabu yao kuendeshwa kisasa, hata hivyo wanachama hao wakapewa mchongo ili wasiingie mkenge na watani zao Simba.

Simba licha ya kupitisha mabadiliko yao na klabu kuendeshwa kwa mfumo wa hisa, lakini bado wamekwama Tume ya Ushindani (FCC) kutokana na baadhi ya mambo kutokuwa sawa, na hilo ndilo lililowafanya vigogo wa zamani wa Yanga kuwatahadharisha wanachama kabla ya mkutano.

Wakizungumza na Mwanaspoti kwa muda tofauti, wenyekiti wa zamani wa Yanga, Lloyd Nchunga na Imani Madega walisema mpaka sasa mchakato wao umezingatia matakwa yote ya FCC, hivyo wanaimani kila kitu kitaenda sawa na kutopata kikwazo, lakini bado wanachama wawe makini.

Nchunga alisema hadi kufikia hatua waliopo sasa kumekuwa na mchakato mrefu wa kufikia hapo huku akiwataka wanayanga watumie nafasi zao katika ngazi za awali juu ya mabadiliko hayo na kuepuka kuchanganywa na baadhi ya wanaonekana kuyapinga kwa sasa kabla ya mkutano huo.

Alisema, mapendekezo ya mabadiliko hayo tayari yametolewa katika rasimu, hivyo ni fursa kwa wanayanga wote kuitumia vyema nafasi hiyo kutokana na mambo mengi kuwekwa wazi.

“Niliona hata elimu imetolewa matawini na wanayanga ambao hawako katika matawi wajitahidi kupokea maoni yao ili kufanikiwa inahitajika mawazo ya kila mtu kuyapokea na kuyafanyia kazi,”

Advertisement

alisema Nchunga na kuongeza, Kamati inayoratibu mchakato huo chini ya Wakili Msomi Alex Mgongolwa imefanya kazi kubwa na kila kitu kitaenda sawa kupitia mkutano huo muhimu unaotambulika kikatiba.

“Hao wazee waliosema wanapinga mabadiliko ni haki yao kusema hivyo, lakini bado wanayanga ni lazima wahakikishe wanaikomboa klabu yao kutoka ilipo kwenda kwenye maendeleo ya kweli,” alisema Nchunga na kusema hata yeye wakati akiwa Yanga mabadiliko ilikuwa dhamira yake kubwa lakini haikuweza kufanyika.

Kwa upande wa Madega alisema kwa kuwa mchakato wao umezingatia zaidi matakwa na masilahi ya klabu na ndio maana asilimia 49 zinagawanywa kwa wawekezaji watatu hadi wanne huku 51 zikisalia kwa wanachama ambao ndio wenye klabu yao ni wajibu wao kuridhia mabadiliko hayo.

“Ukishampa mwekezaji asilimia 49 umempa nguvu kubwa ya maamuzi ndani ya timu yenu na ndio maana sisi Yanga hili hatulitaki kabisa tumezigawanya kwa watu wanne ili kila mmoja apate asilimia 12,” alisema Madenga aliyeongeza kwa kusema anaamini Jumapili hakutakuwa na vikwazo vya aina yoyote ile kwa kuwa kila jambo wamelifanya kwa kufuata taratibu ikiwemo Kamati yao ya mabadiliko iliwajumuisha wanayanga wenyewe.

Advertisement