Wambura ang’ang’aniwa

Michael Wambura.
Muktasari:
- Mayenga amedai kuenguliwa kwake ni njia na mpango wa Kamati ya Uchaguzi wa FAM kumbeba mgombea mwenzake (Wambura).
ZENGWE dhidi ya Michael Wambura, anayewania Uenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mara (FAM) limeanza baada ya Mgombea aliyeenguliwa katika Uchaguzi wa chama hicho Valence Mayenga kupinga kuenguliwa kwake.
Mayenga amedai kuenguliwa kwake ni njia na mpango wa Kamati ya Uchaguzi wa FAM kumbeba mgombea mwenzake (Wambura).
Mayenga alienguliwa katika mchakato huo kwa hoja ya kukosa uzoefu wa kutosha, lakini amepinga hoja hiyo na kudai kuwa wasifu wake unaonyesha kabisa amewahi kufanya kazi kwenye soka kwa zaidi ya miaka mitano kama katiba inavyoelekeza.
“Nimeenguliwa kwasababu ambazo hazina mashiko, wasifu wangu unaonyesha kuwa nimewahi kuongoza soka kwa zaidi ya miaka mitano, nadhani kuna mkakati wa kumbeba Wambura (Michael),” alilalama Mayenga.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Uchaguzi wa FAMA, Wakili Ostack Mligo alisema Mayenga alienguliwa kwa kushindwa kuutetea wasifu wake jambo ambalo liliweka mashaka kama anaweza kubeba dhamana ya uongozi wa chama hicho.
“Unaweza kuwa na wasifu mzuri, lakini ukishindwa kuutetea tunapata mashaka kama ni wa kwako, hicho ndicho kilichotokea kwa Mayenga, anaonekana hana uzoefu wa kutosha.
“Kuhusu hoja ya kipengele cha kuwa mkazi wa mkoa wa Mara inategemea na tafsiri, yawezekana ameshindwa kukitafsiri vizuri lakini ukweli ni kwamba Wambura amekidhi vigezo vyote vya kikatiba,” alifafanua Mligo ambaye alionekana kuwa makini.