Wakali hawa wamewahi kucheza timu moja

Muktasari:
Hata hivyo, huo ndio ukweli. Hawa hapa ni wachezaji ambao huwezi kuwafikiria kabisa kama waliwahi kucheza timu moja kwenye maisha yao ya soka. Unachokiona ndicho chenyewe, wakali hawa walikipiga timu moja huko nyuma.
LONDON, ENGLAND . KUNA wachezaji waliwahi kucheza timu moja kiasi cha kuzoweana na kufanya kuwa ngumu kumtaja mchezaji mmoja bila ya mwingine.
Kwa mfano, Xavi na Iniesta. Rio Ferdinand na Nemanja Vidic. Emery Heskey na Michael Owen. Hiyo ni kwa kuwataja kwa uchache tu, kwamba walikuwa na muunganiko mzuri walipokuwa wakicheza timu moja kwenye mchezo wa soka.
Lakini, kuna wachezaji hao wala huwezi kudhani kama waliwahi kucheza timu moja. Hivyo, inapotokea kuona wamepiga picha wakiwa na jezi za timu moja ni kitu kinachokufanya ushtuke na pengine unaweza usiamini unachokiona.
Hata hivyo, huo ndio ukweli. Hawa hapa ni wachezaji ambao huwezi kuwafikiria kabisa kama waliwahi kucheza timu moja kwenye maisha yao ya soka. Unachokiona ndicho chenyewe, wakali hawa walikipiga timu moja huko nyuma.
Robert Pires na Ashley Young (Aston Villa)
Wakati Robert Pires anajiunga na Aston Villa mwanzoni mwa msimu wa 2010/2011, tayari alikuwa nyakati zake zinaanza kumtupa mkono. Kipindi hicho Ashley Young ndio uliokuwa wakati wake wa kutamba kwenye soka na hakuchukua muda akanaswa na Manchester United kwa ada ya Pauni 17 milioni. Man United walifaidi huduma ya Young kwa miaka mingi na kuachana naye mwaka jana tu hapo. Katika kikosi cha Aston Villa, Pires alikwenda kucheza kwenye namba 10, akionyesha ubora mkubwa na kuisaidia timu hiyo kumaliza ligi kwenye nafasi ya tisa.
Fabinho na Cristiano Ronaldo (Real Madrid)
Maisha ya Fabinho kwenye kikosi cha Real Madrid yalikuwa ya muda mfupi sana. Mbrazili huyo alikwenda Santiago Bernabeu kucheza kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea Rio Ave ya Ureno. Baada ya kutamba kwenye timu B, akapata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza na kutumika katika mchezo dhidi ya Malaga, ambapo Los Blancos ilishinda 6-2. Kwenye mchezo huo, Real Madrid ilikuwa na mastaa kibao akiwamo Luka Modric, Mesut Ozil na Cristiano Ronaldo, hivyo kumfanya Fabinho kuwa na nafasi ya kucheza timu moja na wakali hao.
Louis Saha na Alan Shearer (Newcastle)
Straika Louis Saha aliwahi kutamba kwenye vikosi vya Fulham, Manchester United na Everton kwa kuvitaja kwa uchache. Lakini, kwenye soka lake aliwahi kutamba pia kwa mkopo katika kikosi cha Newcastle United alipocheza kwa mkopo. Akiwa huko Newcastle United, Saha alipata nafasi ya kucheza pamoja na straika moto kabisa, Alan Shearer, aliyekuwa kiboko kwa kutupia. Hata hivyo, maisha ya Saha huko St James’ Park hayakuwa matamu sana, alifunga bao moja tu.
George Weah na Shaun Wright-Phillips (Man City)
George Weah kwa sasa ni Rais wa Liberia. Lakini, huko staa mkubwa kwenye soka na kuwa Mwafria pekee aliyeshinda tuzo ya Ballon d’Or. Alikuwa mchezaji mkubwa sana akitamba huko Ulaya. Lakini, utashangaa aliwahi kucheza timu moja, kwa kipindi cha miezi miwili na kinda aliyekuwa akichipukia wakati huo, Shaun Wright-Phillips huko Manchester City. Jambo hilo limemfanya Wright-Phillips kuwa kwenye orodha ya wachezaji waliowahi kucheza pamoja na rais huyo wa Liverpool kipindi hicho alipokuwa akitamba Ulaya.
Mikael Silvestre na Ronaldo (Inter Milan)
Beki Mfaransa, Mikael Silvestre alitamba kwa msimu mmoja kwenye kikosi cha Inter Milan kabla ya kuigomea Liverpool na kwenda kusaini kuichezea Manchester United mwaka 1999. Wakati Silvestre akiwa Inter Milan, kipindi hicho kwenye kikosi cha San Siro kulikuwa na straika moto wa Kibrazili, Ronaldo de Lima, akifanya mambo yake ya kuwatesa mabeki. Hilo lilimfanya Silvestre kupata nafasi ya kucheza na kufanya mazoezi pamoja na Ronaldo kwenye kikosi hicho cha Inter Milan.
Pierre Emerick Aubameyang na Eden Hazard (Lille)
Huko nyuma kabla ya kucheza soka la kiwango cha juu na kutangaza majina yao kuwa masupastaa wakubwa kwenye mchezo wa soka, Pierre Emerick Aubameyang na Eden Hazard walikuwa kwenye kikosi kimoja cha Lille ya Ufaransa. Wakati Hazard akitamba na kikosi hicho katika msimu wa 2009/2010, Aubameyang alikuwa ametua kwenye timu hiyo kwa mkopo akitokea AC Milan na hapo Lille pakawa pamenoga zaidi. Hata hivyo, mambo hayakuwa mzuri kwa Aubameyang ambapo aliishia kucheza mechi mbili tu kwa msimu mzima wa Ligue 1.
Sol Campbell na Andy Carroll (Newcastle)
Baada ya kukipiga kwenye kikosi cha Notts County na kisha kurejea kwa muda mfupi huko Arsenal, beki wa kati Sol Campbell alikwenda kuichezea Newcastle United. Wakati akienda kujiunga na kikosi hicho cha St James’ Park, Campbell alipokelea na straika mwenye kimo chake na nywele ndefu, Andy Carroll. Jambo hilo liliwafanya wawili, wachezaji walionekana kuwa katika zama mbili tofauti wakajikuta wakicheza timu moja. Carroll aliingia kwenye rekodi ya kuwa mmoja wa wachezaji waliosajiliwa kwa pesa nyingi na Liverpool, aliponaswa kwa Pauni 35 milioni Januari 2011.
Serge Gnabry na Darren Fletcher (West Brom)
Kitu cha kwanza, Serge Gnabry na Darren Fletcher ni wanasoka waliotokea kwenye zama tofauti. Lakini, waliwahi kucheza timu moja na mtu aliyewafanya wawili hao kuwa kwenye timu moja ni kocha Tony Pulis. Hata hivyo, kocha Pulis, hakuwapa wakati unaostahili Gnabry na Fletcher kwenye kikosi chake cha West Brom. Gnabry akaondoka na sasa anatamba huko Bayern Munich, huku Fletcher, baada ya kuachana na Baggies alienda kujiunga na Stoke City na sasa anajifunza ukocha.
Marko Arnautovic na Mario Balotelli (Inter Milan)
Wakati wawili hao wote wakiwa wasumbufu wakubwa kwenye vyumba vya kubadilishia, hivyo inaonekana kama ni maajabu kwa Inter Milan kuweza kuwamudu wachezaji hao, hasa msimu wa 2009/10, ambapo walibeba ubingwa wa Ligi Kuu England. Katika msimu huo, Arnautovic hakuwa akipata nafasi sana kwenye kikosi cha kocha Jose Mourinho, kwa sababu alidai kwamba alikuwa na tatizo za kitoto. Kitu kama hicho kilitokea pia ka upande wa Balotelli. Mourinho aliwahi kusema kuhusu Balotelli, kwamba anaweza kuandika kitabu cha kurasa 200 kwa miaka miwili aliyokuwa na straika huyo Inter Milan.
Yakubu na Shkodran Mustafi (Everton)
Beki wa kati, Shkodran Mustafi aliibukia kwenye kikosi cha vijana cha klabu ya Everton, akajifunza chini ya mabeki Phil Neville na Tony Hibbert waliokuwa kwenye kikosi hicho cha Goodison Park kwa wakati huo. Mechi yake ya kikosi cha kwanza akiwa na Everton ilikuwa kwenye Europa League dhidi ya BATE Borisov. Kwa sababu tayari Everton ilikua imeshafuzu, kocha aliamua kupumzisha sehemu kubwa ya wachezaji wake wa kikosi cha kwanza, lakini Yakubu alicheza na hivyo kuwa kwenye timu moja na Mustafi walau kwa dakika 10 ndani ya uwanja.