Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wachezaji 7 Simba wamerogwa?

Muktasari:

Mastraika waliopo klabuni hapo kwa sasa ni Mussa Hassan ‘Mgosi’, Danny Lyanga, Ibrahim Ajibu, Joseph Kimwaga, Hija Ugando, Hamis Kiiza na Raphael Kiongera.

TAKWIMU hazidanganyi. Hali ya washambuliaji wa Simba inaonekana kuwa mbaya katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita ambapo timu hiyo imecheza michezo minane ya mashindano ambapo imeshinda mitatu tu.

Tangu Ligi Kuu Bara ilipoendelea Desemba 12 mwaka jana, Simba imecheza mechi nne za ligi hiyo na kushinda moja kabla ya kwenda visiwani Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi ambapo ilicheza mechi nne na kushinda mbili tu huku washambuliaji wake wa kati wakizifumania nyavu mara moja tu katika michuano hiyo.

Simba iliondoshwa na Mtibwa Sugar juzi Jumapili kwa kipigo cha bao 1-0.

Kutokana na ubutu wa safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, Kocha Dylan Kerr amekuwa akifanya mzunguko wa wachezaji wa kuwapa nafasi mastraika wake wote saba katika mechi tofauti tofauti.

Mastraika waliopo klabuni hapo kwa sasa ni Mussa Hassan ‘Mgosi’, Danny Lyanga, Ibrahim Ajibu, Joseph Kimwaga, Hija Ugando, Hamis Kiiza na Raphael Kiongera.

Simba ilipopata sare ya mabao 2-2 na Azam Desemba 12 mwaka jana, nuru ilianza kung’aa kwa Lyanga aliyeichezea Simba mechi yake ya kwanza siku hiyo hivyo kujipatia nafasi ya kudumu katika kikosi na kucheza mechi zote nane (moja akitokea benchi) lakini amefunga bao moja pekee katika michezo hiyo jambo ambalo limeifanya safu ya ushambuliaji kuwa butu zaidi.

Katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ni Ajibu pekee aliyefunga mabao mengi akiwa amefunga manne katika mechi mechi hizo nane ambapo alianza mara nne na nne nyingine akitokea benchi.

Hali inaonekana kuwa ngumu kwa Kiongera ambaye amerejeshwa Simba akitokea KCB ya Kenya alikokuwa akicheza kwa mkopo, kwani tangu alipoanza kupewa nafasi dhidi ya Toto Africans ya Mwanza kisha kucheza mfululizo hadi kwenye kombe la Mapinduzi, ameshindwa kuwa na hatari yoyote kwa wapinzani na kuambulia patupu akiwa hajafunga bao lolote mpaka sasa.

Nahodha wa timu hiyo, Mgosi ambaye aliibuka Mfungaji Bora wa Ligi Kuu na Simba mwaka 2010, ameshindwa pia kuifungia timu hiyo bao lolote katika michezo sita kati ya minane aliyocheza katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita huku sababu kubwa ikiwa ni kuchezeshwa pembeni nafasi ya  winga badala ya straika wa kati.

Kiiza aliyeanza kwa kasi Msimbazi akifunga mabao manane katika mechi tano kabla ya mapumziko ya ligi, amejikuta akishindwa kurejea katika makali yake baada ya kucheza mechi saba bila kufunga bao hata la kuotea huku akionekana kupooza.

Kocha Kerr amejikuta katika wakati mgumu zaidi baada ya chipukizi Hija Ugando na Kimwaga ambao wamecheza katika mechi chache wakishindwa kufanya miujiza.

Yanga nafuu. Hali inaonekana kuwa nafuu kidogo upande wa Yanga ambapo katika mastraika wake watano ni Matteo Saimon pekee aliyeshindwa kufunga bao katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita. Matteo amecheza mechi moja tu katika kipindi hicho.

Tambwe ndiye kinara wa mabao katika safu hiyo akiwa amefunga mabao sita katika mechi nane za mwisho alizocheza ikiwamo mabao matatu ‘Hat Trick’ aliyofunga dhidi ya Stand United.

Mzimbabwe, Donald Ngoma amefunga mabao mawili katika mechi hizo wakati washambuliaji wengine, Malimi Busungu na Paul Nonga wakifunga bao moja moja.

Kiungo Thaaban Kamusoko amesaidia katika kufuta makosa ya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo akifunga mabao matatu katika mechi hizo nane ikiwemo bao pekee la ushindi dhidi ya African Sports jijini Tanga.