Vyuma vimekaza! Nenda kwa Mwanaheri

Muktasari:
Tangu nimeanza hadi sasa naweza kusema imenilipa na nina furaha na kazi yangu ambayo natumia akili kuingiza fedha inayoniweka mjini,” anasema.
SUPASTAA wa kike kwenye tamthilia ya Kapuni, Mwanaheri Ahmed wala hanaga presha kabisa kwenye mishemishe zake za kutafuta chapaa.
Anajua kutumia shahada yake ya masuala ya bima katika kuingiza mkwanja wake kihalali kabisa huku akiendesha mambo yake kisasa kupitia sanaa.
Tofauti na wasanii wengine, Mwanaheri anafichua kuwa sanaa inalipa na ndio sababu anaendelea kutumia muda wake mwingi kwenye tasnia hiyo.
Licha ya kuwepo kwa maharamia wa kazi za wasanii, lakini hilo halijawa tatizo kabisa kwa Mwanaheri, ambaye huko kwenye Kapuni anakiwasha kwelikweli.
“Kazi ya sanaa inanilipa na ndio maana naendelea kuifanya, ingekuwa hainiingizii kipato sidhani kama ningeendelea kujishughulisha nayo. Tangu nimeanza hadi sasa naweza kusema imenilipa na nina furaha na kazi yangu ambayo natumia akili kuingiza fedha inayoniweka mjini,” anasema.
HACHAGUI PAKULA
Ni mara chache unaweza kumuona msanii maarufu kajichanganya na jamii inayomzunguka hasa katika suala la chakula, Mwanaheri kwake freshi tu.
“Mimi ni mtu wa kawaida sana, naishi kama wanavyoishi Watanzania wenye hali ya chini.
“Huwezi amini nakula vyakula vya jumuiya naweza kuingia kwa mama ntilie nikala kama kawaida,” anasema.
WAHUNI SIO WATU WAZURI
Kuna msemo uliozoeleka kuwa mtu akitoka mkoani lazima aumizwe ikiwa na maana kwamba anaingizwa mjini kwa kuibiwa basi unaambiwa Mwanaheri kakutana na mtihani huo.
“Umenikumbusha mbali sana nimeshawahi kuingizwa mjini huwezi kuamini nakumbuka mwaka wa kwanza naingia chuo niliingizwa chaka na dalali, ambaye aliniambia nimtumie kodi ili akanilipie kwa mwenye nyumba,” anasema.
“Nilivyokuwa naanza chuo sikupata nafasi hosteli nikaamua kutafuta chumba cha kwangu mwenyewe lakini sikufanikiwa hata kukaa kwani nilitapeliwa fedha yangu yote,” anasema na kuongeza;
“Siwezi kukumbuka ilikuwa kiasi gani kipindi hicho lakini kikubwa naweza kusema niliingizwa mjini na simu nilizimiwa nikajikuta natamani kurudi nyumbani na kuachana na chuo kwani nilitumia kiasi kikubwa cha fedha,” anasema.
ANA DEGREE YA BIMA
Basi kama ulikuwa unamchukulia poa Mwanaheri kutokana na kumuona kwenye Kapuni, basi unajidanganya kwani ni msomi mwenye shahada yake buana.
“Nina shahada ya bima niliyoipata Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) lakini kwa mapenzi na kuigiza niliamua kuweka pembeni fani hiyo kwa muda ili kujikita huku,” anasema na kuongeza;
“Katika tasnia hii ambayo imekuwa ikiniingizia fedha napoteza muda, ikitokea nikaamua kutumia elimu yangu basi naweza kurudi huko kwa kutafuta kazi,” anasema.
RIYAMA AMEMPA UMAARUFU
Alipokuwa anaanza kujihusisha na tasnia hiyo mijadala mingi iliibuka kwa mwanadada huyo kufanananishwa na Riyama Ali kutokana na umbo lake na kimo kuendana na mkongwe huyo.
“Sizani kama tunafanana sana, kwa upande wangu nachukulia kawaida ila kwa namna moja au nyingine amesaidia kunikuza kisanaa kwani ndio mwanzo wa watu kunifuatilia,” anasema.