Vurugu Maseke, Elias chanzo ni hiki

Muktasari:

  • Tukio lililowashangaza wengi lilitokea dakika ya 42 na kipa huyo alimtupia ngumi kiungo huyo, kabla ya Elias kujibu napigo na kuamuliwa, huku mwamuzi wa mchezo huo, Omari Mdoe kutoka Tanga akishindwa kutoa adhabu yoyote.

Kipa wa KMC, Wilbol Maseke ameomba radhi kutokana na ugomvi wake dhidi ya kiungo wa  timu hiyo, Ibrahim Elias kwenye mchezo dhidi ya Yanga, jana Jumamosi Februari 17 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, huku akidai hakuwa sawa.

Tukio lililowashangaza wengi lilitokea dakika ya 42 na kipa huyo alimtupia ngumi kiungo huyo, kabla ya Elias kujibu napigo na kuamuliwa, huku mwamuzi wa mchezo huo, Omari Mdoe kutoka Tanga akishindwa kutoa adhabu yoyote.

Kipa huyo alionekana kutokuwa sawa kwenye mchezo huo ambao alisababisha bao la kwanza kwa kushindwa kutoa pasi sahihi kwa beki wake kabla ya kunaswa na nyota wa Yanga na katika piga nikupige, kiungo Yahaya Mudathir akafunga bao la kwanza sekunde chache baada ya mchezo kuanza.

Tukio hilo lilionekana kumchanganya kipa huyu na hivyo kutokuwa sawa ndipo Elias alitaka kuongea naye lakini akaambulia kichapo kabla ya kumrudishia na wawili hao kuamuliwa. Hata hivyo kipindi cha pili Maseke alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Denis Richard.

Katika ukurasa wake wa Instagram, Maseke aliomba radhi akiandika "Poleni sana mashabiki zangu na wanaopenda kazi ninayoifanya nikiwa uwanjani, pia niombe radhi kwa kilichojitokeza mimi kugombana na mwezangu, sio kusudio, pia baada ya hapo ukweli ni kwamba sikuendelea na ugomvi 'dressing room' bali yale ni maamuzi ya mwalimu kunitoa nimeheshimu hilo."
"Lakini nina mengi ya kusema ambayo huwa yanaendelea nje ya uwanja, ambayo yalisababisha kuharibu saikolojia yangu, lakini kwa leo niishie hapo na kusema naomba mnisamehe kwa kilichotokea."

Katika mchezo huo ambao KMC ilikuwa nyumbani kwenye uwanja huo, ilikumbana na kichapo cha mabao 3-0 na kuiacha Yanga ikiendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa pointi 43, ikiwa ni mchezo wa kwanza wa mzunguko wa pili.

Mabao ya Yanga kwenye mchezo huo yalifungwa na Mudathir (2) na Pacome Zouzoua huku mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara wakionyesha kiwango safi mbele ya KMC ambao kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza walipoteza tena kwa mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, jijini Dar es Salaam.