Vita ya Mayele v Inonga, Onyango

ILIKUWA ni shoo shoo kwa mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele na mabeki wa Simba, Joash Onyango na Henoc Inonga Baka kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi ambao ulimalizika kwa timu hizo mbili kugawana pointi kwa matokeo ya 0-0.
Wadau wengi kabla ya mchezo huo, walikuwa wakiizungumzia bato ya Mayele na Inonga kutokana na ahadi ambayo awali aliitoa mshambuliaji huyo wa Yanga kwamba alikuwa na deni la kuifunga Namungo na Simba ambao alikutana nao kwa mara ya pili Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mwanzoni mwa mchezo huo, Mayele alionekana kutosimama eneo moja na badala yake alikuwa akijaribu kutanua kuona kama anaweza kutengeneza mianya kwa Saido na Feisal ili kupenya lakini mpango huo ulionekana kushindikana kwani kila ambapo alikuwa akitua mabeki wa Simba walikuwa makini.
Yapo matukio manne ambayo Mayele alihusika nayo kwenye mchezo wa jana, la kwanza lilikuwa lile la dakika ya 12 ambapo alipenyezewa pasi, akiwa kwenye mikimbio yake huku akionekana anaenda kuleta madhara kwa Simba, Inonga alimzidi maarifa mshambuliaji huyo na kuondoa hatari hiyo kwa kuingia uvunguni na kuchukua mpira.
Inonga alionekana kuwa mwenye tabasamu baada ya kuona kuwa ametimiza kile ambacho alilenga, dakika ya 20, Mayele alihusika kwenye tukio jingine ilikuwa ni baada ya kuchongwa krosi, akiwa kwenye eneo la hatari alishindwa mshambuliaji huyo kuuweka mpira kwenye himaya yake.
Dakika ya 32 na 39, Mayele alihusika kwenye matukio mengine ambayo pia hayakuwa na madhara kwa Simba kwani Onyango na Inonga ni kama walijua namna ya kukabiliana na mshambuliaji huyo.
Inawezekana kuwa hii ndio ilikuwa nafasi bora zaidi kwa Mayele kwani dakika ya 71, baada ya kazi nzuri ya Feisal Salum akiwa na Onyango, mshambuliaji huyo mwenye mabao 12 aliiwahi pasi ya mbele na kupata mwanya ambao aliutumia kutandika shuti kali ambalo hata hivyo halikuwa na macho likapiga nyavu za nje.
Ili kufanya majaribio mengine ya kuifunga Simba kwenye ligi, itambidi Mayele kusubiri hadi msimu ujao maana hakuna tena uwezekano wa vigogo hao kukutana katika Ligi Kuu kwani katika michezo yote miwili wametoka suluhu. Mayele aliifunga Simba 1-0 katika mechi ya ufunguzi wa msimu huu ya Ngao ya Jamii.